UHALIFU HAUKUBALIKI:Taasisi nyingi sana siku hizi zimeingiliwa na makanjanja hata makanisani, misikitini, vyombo vya dola, wanasiasa kote makanjanja...

NA DIRAMAKINI

LEO Septemba 30, 2022 wadau mbalimbali wameshiriki mjadala muhimu na maalum wa Kitaifa ambao uliangazia juu ya usalama nchini na operesheni mbalimbali za Jeshi la Polisi.
Mjadala huo ambao umerushwa mubashara na vyombo mbalimbali vya habari kupitia Mtandao wa Zoom umeratibiwa na Watch Tanzania ambapo wachangia mada wamesema haya;

SACP. DAVID MISIME, MSEMAJI WA JESHI LA POLISI

"Majukumu makubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda maisha ya watu na mali zao pia kukamata, kupeleleza na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, haya yote huwezekana kutokana operesheni mbalimbali kupitia doria baada ya kupata taarifa za watuhumiwa kutaka kufanya matukio mbalimbali.
"Matukio ya kiuhalifu mara nyingi hutokea mitaani ambako kuna makazi ya watu, hivyo Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuwatambua wahalifu mbalimbali katika maeneo yao na hasa kwa watu wasiowatambua wakizunguka na kuzurura bila utaratibu na kuonesha ishara ya mashaka.
"Operesheni nyingi huwa za siri maana wahalifu nao hawapendi kukamatwa wanataka matukio yao yafanikiwe hivyo mara nyingi tunaendesha operesheni hizi kwa siri ila tukishirikisha na wadau wachache ambao wanaweza kutupa taarifa za watuhumiwa, huwezi kuuza ramani ya vita na kutarajia kushinda hivyo lazima iwe siri,"amesema.

ZUBERI S. CHEMBERA, NAIBU MKURUGENZI WA UPELELEZI WA MAKOSA YA JINAI ZANZIBAR
"Kwa upande wa Zanzibar iko shwari wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato, hivyo nitoe pongezi za dhati kwa Rais wa Zanzibar kuhakikisha nchi ni tulivu na shwari hili limetokana na uimara wa Jeshi la Polisi na wadau shirikishi.

"Diplomatic Polisi ni kikosi kazi chenye mchanganyo wa askari wote au vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika visiwa vya Zanzibar, lengo likiwa kuunganisha nguvu kusudi kila rasilimali tuliyonayo tunaitumia ili kuhakikisha ulinzi na usalama unataradadi Zanzibar.

"Zanzibar imezungukwa na maji katika pembe zake zote, hivyo moja ya mkakati ni kuhakikisha tunashirikiana na mikoa yote ya mwambao wa Hindi unayotuzunguka kama Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara hivyo tumekuwa tukifanya vikao na operesheni mbalimbali kuhakikisha usalama wa wananchi,"amesema.

RPC. LONGINUS A. TIBISHUBWAMU, KAMANDA WA POLISI MKOA WA MARA
"Kwa sasa Mkoa wa Mara upo shwari kutokana na operesheni mbalimbali zinazoendelea ingawa kwa kipindi cha mwezi Septemba yalitokea matukio matatu ya unyang'ang'i wa kutumia silaha katika wilaya ya Serengeti na Butiama ila kwa sasa hakuna shida hiyo tena.
"Kwenye matukio hayo matatu yaliyotokea Jeshi la Polisi kwa kutumia intelligence yake na msako mkali wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne pamoja ya buduki aina ya G3 na risasi 6, baada ya kuyahoji haya majambazi yalikiri kuhusika katika matukio yote matatu na kuwapeleka askari sehemu walipoficha hizo silaha,"amesema.

BISHOP BENSON BAGONZA, ASKOFU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT)
"Maadili yanaanza kwenye familia zetu, hivyo wazazi tujitahidi sana katika kuimarisha malezi ya watoto wetu tukifanikiwa katika hili uhalifu utapungua kwa sababu jamii imefunzwa maadili mema ya kujua kipi kibaya kipi kizuri.

"Taasisi nyingi sana siku hizi zimeingiliwa na makanjanja hata makanisani, misikitini, vyombo vya dola, wanasiasa kote makanjanja wapo wengi sana ambao wanapotosha ukweli kwa maslahi yao binafsi,"amesema.

WAMBURA IGEMBYA, KATIBU WA UVCCM MKOA WA MARA

"Niwaombe wanasiasa kutokujihusisha kwa namna yeyote ya kufurahishwa na uhalifu unaoendelea katika maeneo yetu tuwape ushirikiano wa kutosha Jeshi la Polisi katika kuwavumbua wahalifu katika maeneo yetu kusudi taifa liwe na amani na utulivu.
"Ulinzi shirikishi ni jambo jema sana kukiwa na ushirikishwaji kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama nchi yetu itakuwa tulivu na ninauhakika uhalifu utapungua kama sio kuisha kabisa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news