CWT yaonya wenye tabia za kuwaonja wanafunzi

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Walimu (CWT) Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa kimeonya kuwa hakitohusika na utetezi wa walimu watakaojihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu ikiwemo mahusiano ya kingono na wanafunzi.
Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Iringa Vijijini, Mwalimu Simoni Mnyawami akiongea jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Stanslaus Muhongole wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho wilaya ya Iringa Vijijini.

Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Iringa Vijijini Mwalimu Simoni Mnyawami amesema ni aibu kusikia walimu wakitajwa kuhusika katika uhalifu huo huku akisisitiza hatua zaidi za kisheria zichukuliwe ili iwe fundisho kwa watakaobainika.

Mwenyekiti huyo ameyasema hayo wakati wa mkutano mkuu wa CWT baada ya mgeni wa heshima Mkuu wa Wilaya ya Iringa kuwataka walimu kuzingatia weledi wa taaluma kwa kuwafichua wanaojihusisha kingono na wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo akiongongozwa na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Iringa Vijijini, Mwalimu Simoni Mnyawami kutoka kwenye mkutano huo mara baada ya kumaliza kuhutubia.

Mnyawami amesema kuwa, suala la utovu wa nidhamu linapaswa kuheshimuwa kwa kila mwalimu ili kulinda hadhi ya taaluma hiyo ikiwemo utoro, ulevi wa kupindukia pamoja na baadhi ya walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Mwenyeji wa mkutano huo mkuu wa kikatiba Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Iringa Vijijini, Mwalimu Simoni Mnyawami alisema ni muhimu walimu wakatambua na kuheshimu taaluma waliyo nayo kwa kuwa wamepewa dhamana na serikali pamoja na jamii kuwa walezi wa watoto katika kuwajenga kinidhamu na kitaaluma.

Kulingana na changamoto ya utovu wa nidhamu iliyotajwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo aliyekuwa mgeni wa heshima anasema, jambo la walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi halipaswi kufumbiwa macho.
Moyo amewataka walimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wanaowafundisha ili taifa liweze kupata wasomi wengi ambao wanauwezo wa kuja kukisaidia Taifa hapo baadae.

Amesema kuwa, kuna baadhi ya walimu wamekuwa wakiaribu taswira halisi ya kada ya ualimu kwa baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi na kuwafanyia ukatili wanafunzi kwa makusudi hivyo walimu wanapaswa kutoa taarifa kwa mwalimu yeyote atakayekutwa anafanya vitendo vya ukatili.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo akipokea hotuba ya walimu wa Iringa Vijijini wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho.

Amesema kuwa, kazi kubwa ya mwalimu ni kuwafundisha wanafunzi waweze kufaulu na sio kuwafanyia ukatili wanafunzi.

Post a Comment

0 Comments