DC Mboneko:Tuendelee kupata chanjo ya UVIKO-19

NA MARCO MADUHU

MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19, ili kuimarisha kinga za miili yao, na kuepuka kupata madhara makubwa pale watakapoambukizwa virusi vya UVIKO-19.
Kikao cha hamasa chanjo ya UVIKO-19 kikiendelea.

Mboneko amebainisha hayo leo Septemba 7, 2022 wakati akifungua kikao cha uhamasishaji wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 katika Kata Nne za Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambazo ni Lyamidati, Mwenge, Imesela, na Mwamala.

Amesema baada ya watu kupata chanjo ya UVIKO-19 maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua hapa nchini, ambapo mtu akipata chanjo hawawezi kudhurika zaidi tofauti na wale ambao hawakupata chanjo hususani pale watakapopata maambukizi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye kikao cha kuhamasisha chanjo ya UVIKO-19 katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

“Tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea chanjo za UVIKO-19 na kujali afya za wananchi wake, na wananchi wakiwa na afya njema watafanya vizuri shughuli za maendeleo,”amesema Mboneko.

“Wakati wa utoaji chanjo ya UVIKO-19 anzeni pia na Makundi maalum, wakiwemo wazee, wenye magonjwa sugu na watumishi, na pale penye changamoto nipeni taarifa ili tuitatue na zoezi hili lifanikiwa kwa asilimia 100 kwa kuchanja wananchi wengi,”ameongeza.

Katika hatua nyingine Mboneko ameonya upotoshaji juu ya chanjo ya UVIKO-19 na kubainisha kuwa chanjo ni salama na zinatolewa bure, na kuwataka wataalam watoe elimu ya kutosha kwa wananchi ili zoezi hilo lifanikiwe kama ilivyofanyika kwenye chanjo ya Polio.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Nuru Yunge, amesema wamefanya kikao hicho cha kampeni ya kuhamasisha chanjo ya UVIKO-19 kwa kushirikiana na Shirika la USA PeaceCorps kwa kuanza na Kata Nne wilayani humo.
Amesema katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga lengo lao lilikuwa ni kuchanja watu chanjo ya UVIKO-19, 218,929 lakini watu waliopata chanjo kamili wilayani humo ni 120,107 na waliopata dozi moja ni 47,359.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news