DKT.KIRUSWA AIAGIZA GST NA STAMICO KUFANYA TAFITI ZA MADINI MUFINDI NA KILOMBERO

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufanya tafiti za madini katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro na wilaya ya Mufindi mkoani Njombe kwa lengo la kubaini aina ya madini yaliyopo katika wilaya hizo.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Kiruswa wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Kilombero Abubakari Asenga katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameainisha maeneo mbalimbali yenye madini ya dhahabu na vito katika wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.

Akijibu swali hilo amesema, Taasisi ya GST imefanya utafiti wa awali sambamba na kuchora ramani kwenye maeneo yote yaliyopo katika Jimbo la Kilombero katika mfumo wa Quarter Degree Sheet (QDS).

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, tafiti za awali zilizofanyika katika wilaya ya Kilombero, zilionesha uwepo wa madini ya dhahabu na madini ya vito katika Kata ya Chisano.

Ameongeza kuwa, GST ilifanya utafiti wa awali na kuchora ramani ya eneo la Hifadhi ya Milima Udzungwa na maeneo jirani ambapo utafiti wa madini uliofanyika katika maeneo hayo hauoneshi taarifa zozote za uwepo wa madini ya thamani katika milima hiyo.

Mkoa wa Morogoro umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini ikiwemo dhahabu, Shaba, Kinywe, madini ya viwandani (Ulanga, Kaoline), madini ya ujenzi (mchanga, kifusi) na madini ya vito ( Rubi, Rodolite).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news