TUUNGANE NA UGANDA:Hatuingilii yao, wenyewe watajijua

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Jamhuri ya Uganda imegundua kiasi kikubwa cha mafuta. Ili kuvuna nishati hiyo imekubaliana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujenga bomba la kusafirisha mafuta hayo kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga jijini Tanga,Tanzania ili kuuzwa nje.

Picha na The Monitor.

Mradi huo unaotekelezwa kwa pamoja na kampuni za China National Offshore Oil Corporation na TotalEnergies kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Mafuta la Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), utagharimu zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 10 na unatarajiwa kukamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2025.

Hivi karibuni, Bunge la Ulaya limepiga kura kupinga utekelezaji wa mradi huo kwa madai kwamba unaharibu mazingira nchini Uganda.

Ni wazi kuwa, hizi ni mbinu zinazotumika na baadhi ya mataifa ya kigeni, kukwamisha jitihada za nchi za Afrika kushirikiana kujikwamua kiuchumi. Uganda imelaani hatua ya Bunge hilo na kusisitiza kwamba utekelezaji wa mradi huo uko palepale.

Mshairi wa kizazi kipya, Bw.Lwaga Mwambande (KiMPAB), anaunga mkono msimamo wa Uganda na kuitaka Tanzania kutoa tamko lake pia. Endelea kufaidi uchambuzi huu kwa njia ya ushairi hapa chini;


1.Kazi ni kupiga vita, tusiweze jikwamua,
Wanauleta utata, kwamba sana watujua,
Kwamba ya kwetu mafuta, tusiweze kuyavua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

2.Kwao wakifanya yao, ni mengi tunayajua,
Hatuingilii yao, wenyewe watajijua,
Yetu wajifanya yao, wakati tunawajua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

3.Vita hii kwetu kubwa, ni sisi kuitatua,
Hata wafanye makubwa, kutaka kutubutua,
Masikio yakizibwa, ndipo vema watajua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

4.Twataka maendeleo, giza tulione jua,
Mafuta ni matokeo, tukatunishe kifua,
Tushike zetu koleo, tutakalo twalijua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

5.Kuna watu wanacheka, waziwazi twawajua,
Pengine cheche wapika, yetu waweze tibua,
Yao kwetu takataka, tukitakacho twajua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

6.Bomba hili la Mafuta, faida tunazijua,
Vile bei ya mafuta, sote sisi twaijua,
Vile huku tumepata, mbele yatatuinua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

7.Ona wajidaidai, mazingira wanajua,
Wakati tunawadai, uchafuzi waibua,
Shingoni tunazo tai, tunakokwenda twajua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

8.Hili Bomba la Mafuta, lianziako twajua,
Uganda kwenye mafuta, wingi wake tunajua,
Hilo litapitapita, Tanzania twatambua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

9.Licha ya hayo mafuta, bidhaa tunaijua,
Mambo mengi tutapata, uchumi kuuinua,
Na watu watatakata, na maisha kuinua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

10.Wilaya makumi kumi, litakopita twajua,
Moto wala hatuzimi, tumekwishajitambua,
Na mradi haukomi, Tanga tutauanua,
Tuungane na Uganda, kulaani watu hawa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news