Filamu ya 'Tanzania:The Royal Tour' iliyotafsiriwa Kijapan yazinduliwa Japan

NA MWANDISHI WETU

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism Expo) yanayofanyika nchini humo kuanzia tarehe 22 hadi 25 Septemba 2022 kuzindua filamu ya “The Royal Tour” iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kijapan.
Sehemu ya Filamu ya "The Royal Tour" ikimuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa akiapa kushika wadhifa huo.

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa maoenesho hayo uliofanyika jana tarehe 22 Septemba 2022, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda aliwasihi washiriki wa maonesho hayo kuiangalia filamu ya “The Royal Tour” ambayo inavionesha vivutio vya Tanzania kama vile hifadhi za taifa za wanayamapori, milima na fukwe za kuvutia kwa ufasaha.

Balozi Luvanda aliwaeleza kuwa tukio hilo la uzinduzi wa filamu limefanyika katika kipindi kizuri ambapo dunia inaanza kufunguka kutokana na masharti ya kusafiri baina ya nchi kupunguzwa, kufuatia kupungua kwa mambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona duniani.
Wageni wanaotembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii yanayoendelea nchini Japan wakiangalia Filamu ya "The Royal Tour".

“Ni matumaini yangu kuwa washiriki wa maonesho haya na wageni wengine, mtapanga safari za kutembelea Tanzania kujionea wenyewe vivutio vya utalii mnavyovishuhudia katika filamu hii na kwenye banda la Tanzania lililopo kwenye Maonesho haya,”Balozi Luvanda alisisitiza.
Wageni wanaotembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii yanayoendelea nchini Japan wakiangalia Filamu ya "The Royal Tour" huku wakiburudika kwa kula vyakula vya Kitanzania.

Tanzania imejipanga kutangaza vivutio vya utalii kwa kutumia majukwaa mbalimbali yakiwemo kama hayo ya Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan ambayo yanashirikisha wadau wengi wa utalii kutoka duniani kote.
Wadau wa Tanzania wanaoshiriki maonesho hayo ni pamoja na; Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news