Rais Dkt.Mwinyi:Tuungane pamoja kuimarisha elimu Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wote kuunga mkono azma ya kuwapatia watoto wote wa nchi hii elimu bora kwa kudumisha upendo, amani na maelewano ili kuweza kupiga vita adui ujinga, maradhi na umaskini na kufikia haraka malengo ya Uchumi wa Buluu.
Mheshimiwa Dokta Mwinyi ameyasema hayo leo katika Uwanja wa Amaan, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha Miaka 58 ya Elimu Bila Malipo, visiwani Zanzibar.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Dokta Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea na azma yake ya kuisimamia kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Buluu ili kutoa fursa kwa wananchi kuweza kunufaika na rasilimali za bahari.
“Nawahakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kutoa mashirikiano katika jitihada zenu za kuwaletea wananchi maendeleo katika kuihudumia jamii na kuwekeza katika sekta ya elimu,”Mheshimiwa Dokta Mwinyi amewahakikishia wananchi juu ya azma njema ya Serikali.

Akitilia mkazo juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora, Mheshimiwa Rais ameeleza nia ya Serikali ya kuifanyia mapitio makubwa Sera ya Elimu ya Mwaka 2006.

Sambamba na hatua ya kuunda Kikosi Kazi Maalum, kwa ajili ya kushauri mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu, ambacho tayari kimekutana na wadau mbalimbali wa ndani na nje wakiwemo wazazi, walimu, wanafunzi, viongozi mbalimbali wakiwemo wastaafu, taasisi za elimu Tanzania Bara, jumuiya zisizo za kiserikali, washirika wa maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Sweden, UNICEF na USAID.
Amebainisha kuwa lengo la mikutano hiyo ni kupata maoni na uzoefu wa wengine katika kuimarisha sekta ya elimu Nchini, mageuzi ambayo yatazingatia pia Mipango mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Malengo ya Dira 2050 ya Zanzibar na ya Dunia, ya Maendeleo Endelevu.

Katika kuhakikisha utekelezaji wa azma hiyo Mheshimiwa Dokta Mwinyi amesema, “Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni wadau wakubwa wa kutoa elimu hapa nchini, kwa hivyo mna wajibu kuungana na Serikali kupitia taasisi mbalimbali kuhakikisha kuwa marekebisho ya Sera ya Elimu na Mitaala yanazingatia mahitaji ya Uchumi wa Buluu na kwamba lengo ni kuwatayarisha vijana wetu kuingia katika Uchumi wa Buluu kwa kuwapa taaluma sahihi itakayowasaidia kupata ajira au kujiajiri wao wenyewe, bila ya kutegemea ajira kutoka Serikali kuu”.
Aidha Dokta Mwinyi ameipongeza Wizara ya Elimu kwa jitihada inazoendeleza kwa dhamira ya kuimarisha shughuli mbali mbali za michezo, Sanaa na utamaduni katika skuli za msingi na sekondari akisema jitihada hizo zinakwenda sambamba na utayarishaji na utekelezaji wa mipango mizuri katika kuimarisha vuguvugu na haiba ya ushindani wa kimichezo kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, hapa nchini.

Pamoja na kupongeza mpango wa kuwaandaa wanafunzi hapa Visiwani kujenga wazalendo, wenye heshima na wenye kuifahamu vyema historia ya nchi, ili hatimae wawe raia wema, Mheshimiwa Dokta Mwinyi ametoa wito kwa wazazi na walezi, kukuza mashirikiano katika kuwapatia fursa na kuwaruhusu vijana kushiriki vyema katika mipango mizuri iliyoandaliwa.
Akikumbusha juu ya umuhimu wa Elimu kwa jamii, Rais Mwinyi amesema, “Serikali yenu inaamini kuwa, ‘Elimu ndio Ufunguo wa Maisha’, Bila ya elimu hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana, kama ambavyo nyinyi mnaamini, kwa hivyo katika kufanikisha dhamira hiyo, ni lazima kila mmoja wetu atekeleze wajibu wake; Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta hii muhimu ili iweze kuwa na wataalamu wa fani mbali mbali na hatimaye kupiga hatua kubwa zaidi za Kimaendeleo”.
Ameongeza kwa kusema, “ninaamini kuwa tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha dhamira hii ya Serikali yenu, inafanikiwa zaidi; hivyo wito wangu kwa wazee, wanafunzi na jamii kwa ujumla, kuitunza miundombinu ya elimu iliyopo na ijayo. Pia, natoa wito kwa wazazi kuitumia vyema fursa iliyopo kwa kuwaandikisha watoto wao skuli, ili tuondokane na udhaifu wa kutojua kusoma na kuandika.

Amesema, “ninawaomba wazazi na walezi mzifuatilie nyendo za watoto wenu, kwa kufuatilia maendeleo yao ya masomo wakiwa skuli, ili waweze kufanya vyema katika masomo yao. Katika hili, lazima yawepo mashirikiano ya karibu baina ya walimu na wazazi kwa manufaa ya wanafunzi wetu na Taifa kwa ujumla; aidha, napenda kuwakumbusha vijana kutokujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani, ili nchi yetu iendelee kubaki salama na waweze kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu”.
Mheshimiwa Dokta Mwinyi amewashauri tena wazazi kuondokana na dhana potofu kuwa mwanafunzi anayeshiriki michezo anapoteza muda wake na hataweza kufanya vizuri katika masomo yake, akisema dhana hiyo si sahihi, ikizingatiwa kwamba hata sayansi inaelekeza kwamba michezo ni sehemu muhimu ya mafanikio ya kielimu kupitia ujenzi wa afya ya mwili na akili, na kama wanavyosema wataalamu, ‘health body, health mind’.

Hivyo Mheshimiwa Dokta Mwinyi amehamasisha jamii kuweka juhudi na uelewa sahihi katika fani hiyo muhimu akisema huenda na kuna kila sababu pia kwa mwanafunzi anayeshiriki michezo akafaulu na kufanya vizuri zaidi katika masomo yake.

Mheshimiwa Dokta Mwinyi ameyashukuru na kuyapongeza Mashirika na Taasisi mbalimbali za Maendeleo, kutoka ndani na nje Nchi, kwa misaada yao katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya Elimu, ikiwemo Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), “Global Partnership for Education”, Milele Zanzibar Foundation, UNICEF, UNESCO, Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), USAID, Serikali ya Watu wa Korea kupitia Shirika la “Good Neighbour”, Shirika la Misaada la Korea ya Kusini (KOICA), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika (BADEA).
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Leila Mohamed Mussa, akimkaribisha Mgeni Rasmi, ameeleza kuwa Tamko la Elimu Bure, lililotolewa na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, ni ithibati ya ujasiri na upeo mkubwa wa Viongozi wa Nchi hii tangu awali, katika kupigania maendeleo ya watu wote, ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Ali Khamis Juma, ameeleza faraja inayozidi kupatikana kutokana na fursa mpya za kuimarisha elimu hapa visiwani zikiwemo za ushirikishwaji wa umma katika kukabiliana na changamoto za utoaji wa huduma hiyo, sambamba na juhudi za kuelimisha kupitia vipindi mbalimbali vya kitaaluma katika vyombo vya Habari.
Akiwasilisha salamu za Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Unguja, Bi. Hamida Mussa Khamis, ameshukuru juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar, ikiongozwa na Rais Dokta Mwinyi, kwa namna inavyokabiliana na na tatizo la uchache wa miundombinu na madarasa, hasa katika maeneo ya Mjini.

Kupitia Risala yao iliyowasilishwa na Mwalim Mussa Abdulrabi kutoka Divisheni ya Michezo, Walimu wamesema licha ya mafanikio makubwa yanayoonekana katika Sekta ya Elimu nchini, ikiwemo Majengo ya Kisasa na Miundombinu bora ya Skuli za Unguja na Pemba, bado kunahitajika mikakati ya kuimarisha nyenzo, huduma na vifaa katika utoaji wa elimu bora hapa visiwani.

Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ya Miaka 58 ya Elimu Bila Malipo Zanzibar ni ‘Uimarishaji wa Miundombinu ya Kielimu ni Chachu katika Kufikia Maendeleo Endelevu’.
Katika Kilele cha Maadhimisho hayo, shughuli mbali mbali zimehusika ambazo ni pamoja na mashindano ya riadha, utenzi, ngonjera na maigizo, burudani, dua, maonyesho yakiwemo ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, na hatimaye kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano tofauti ya Kikanda na Kitaifa.

Maadhimisho ya Siku ya Elimu Bila Malipo ambayo Kilele chake ni kila ifikapo Tarehe 23 Septemba, kama ilivyo desturi yalianza kitaifa tangu mwanzoni mwa Mwezi huu, kwa kuhusisha harakati mbali za kitaaluma na kijamii, makongamano, sambamba na mashindano ya elimu, utamaduni na michezo, kote Unguja na Pemba.
Mawaziri na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Dini, Mashirika ya Kimataifa, Washirika wa Maendeleo, Wazazi, Walimu na Wanafunzi kutoka Skuli, Vyuo na Taasisi za Elimu, Binafsi na Serikali, wamejumuika katika Maadhimisho hayo.

Post a Comment

0 Comments