HGWT:Tunarejesha tabasamu kwa mabinti mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly limeshiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyopo mkoani Mara.
Mkutano huo umefanyika leo Septemba 20, 2022 katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mjini Musoma. Ambapo mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee.

Katika mkutano huo Regina Lucas ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Nyumba Salama Butiama kwa niaba ya Mkurugenzi Rhobi Samwelly aliwasilisha taarifa ya kazi mbalimbali ambazo shirika hilo limekuwa likifanya ikiwemo kutoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukeketaji, ndoa za utoni na aina mbalimbali za ukatili wa Kijinsia kupitia Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama na Nyumba Salama Butiama.

Pia amesema, kazi za shirika hilo ni pamoja na kutoa mahitaji muhimu kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa kijinisia, kuwaendeleza kielimu, kuwapa msaada wa kisaikolojia, kuwafundisha stadi za maisha, kuwafundisha haki zao na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto, Ofisi za Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii katika Wilaya ya Serengeti na Butiama.

Katika utekelezaji wa majukumu hayo shirika limeendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka serikalini kwa lengo la kuhakikisha kwamba ukatili unaisha na watoto wa kike wanalindwa na kuthaminiwa kusudi wafikie ndoto zao kimaisha.
Aidha, Regina amesema kuwa, zipo baadhi ya changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo kama shirika ikiwemo baadhi ya viongozi wa kisiasa katika maeneo wanayofanya kazi kukumbatia mila na desturi zisizofaa.

Pia, kushindwa kukemea ukeketaji jambo ambalo linadhoofisha juhudi za kutokomeza mila hiyo yenye madhara kwa watoto wa kike.

Ameiomba Serikali kuendea kuweka mkazo na kuzidi kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu wanaobainika kujihusisha na kuwafanyia ukatili watoto wa kike hasa kuwakeketa na kuwaozesha katika umri mdogo jambo ambalo linawafanya wasifikie ndoto zao.

Regina amesema, shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kwamba ukatili wa kijinsia haupati nafasi kwani unarudisha nyuma maendeleo.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba amepongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kushirikiana na serikali kwa lengo la kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman ameyataka mashirika yote yanayofanya kazi kuzingatia sheria na taratibu ikiwemo kutoa taarifa kwa wakati.

Pia, Meja Jenerali Mzee ameyataka mashirika ambayo hayana fedha kutoilalamikia Serikali kwamba iyape fedha za kuendeshea shughuli mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news