HOVYOHOVYO EXPRESS:Vile wanatufanyia, hawawezi kurudia

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, abiria wengi nchini wanaotumia vyombo vya usafiri wamekuwa wakidhulumiwa haki zao za msingi sana ambazo wanatakiwa kuzipata pindi watumiapo vyombo hivyo kwa safari mbalimbali.

Pia wengi wamekuwa wakizoea hali tofautitofauti ambazo wamekuwa wakikutana nazo za unyanyasaji na udhalilishaji kama ni za kawaida katika sekta ya usafiri nchini.

Kutokana na changamoto hizo na ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji ambayo imekuwa na mchango na umuhimu mkubwa kwa jamii na Taifa, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha vyombo vyote vya usafirishaji vinafuata miongozo na kanuni mbalimbali ambayo ni rafiki kwa Watanzania wote.

Miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na matumizi ya tiketi za kieletroniki ambayo yamelenga kuwanufaisha wasafirishaji, abiria na Serikali, na kupitia mfumo huo wasafirishaji wanaweza kudhibiti mauzo ya tiketi kwa kuwa mfumo unawawezesha kuona mauzo yote yanayofanyika kupitia simu za mkononi.

Aidha, mfumo huo, unamuwezesha abiria kufanya uchaguzi wa mahali ambapo ataketi kama nafasi hiyo haijachukuliwa na mwingine kupitia malipo ya mtandaoni.

Utaratibu huu na hatua nyinginezo, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema ndizo zitamsaidia abiria kuepuka kupandishwa au kupanda magari au mabasi ya hovyo hovyo, ambayo mwisho wa siku yamekuwa yakiwasababishia maumivu, mateso na hata kuwapotezea muda..., endelea kupitia shairi hapa chini;

1:Ni haki za kisheria, bora tukapigania,
Vile wanatufanyia, hawawezi kurudia,
Wanatujazilizia, hewa tunashindania,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

2:Basi wajichagulia, lile unalijulia,
Siti wajichagulia, dirishani tatulia,
Unataka kutulia, ikibidi kusinzia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

3:Ukisakwa abiria, wapiga debe sikia,
Magoti takupigia, uweze wakubalia,
Tiketi kikupatia, basi ukasubiria,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

4:Basi linapoingia, kituoni tasikia,
Harakisheni ingia, mizigo yenu pakia,
Heshima liyoanzia, taratibu yaishia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

5:Na kwenye basi ingia, tiketi washikilia,
Siti lijichagulia, mwingine amekalia,
Kwingine kumejazia, hata pa kusimamia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

6:Hapo konda kimwambia, kwingine aangalia,
Makusudi mefanyia, pesa ziweze ingia,
Kama hujakazania, jua tajisimamia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

7:Kidijiti kiingia, pale unapolipia,
Siti ikikuambia, basi limeshajazia,
Wazi utaachilia, lingine jitafutia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

8:Sheria kishikilia, haki ukijidaia,
Hapo watakuchukia, njia nzima nakwambia,
Haki utajipatia, mwenyewe tafurahia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

9:Abiria nawambia, mna yenu kisheria,
Vibaya kiwafanyia, nanyi mwawafanyizia,
Serikali nawambia, kifua tawakingia,
Hovyohovyo express, inapaswa kufutika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news