ACT Wazalendo:Bomba la mafuta EACOP liendelee

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelitaka Bunge la Ulaya kuondoa azimio la kutaka kusitishwa kwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Msemaji wa Sekta ya Madini katika chama hicho, Isihaka Mchinjita alieleza hayo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Mchinjita amesema, chama hicho kinalaani maazimio ya Bunge la Umoja wa Ulaya kwa kuwa yanaingilia mambo ya ndani ya Uganda na Tanzania na pia ni ukiukwaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.

“Vitendo hivi vinavyofanywa na Umoja wa Ulaya vinakiuka misingi ya sheria za kimataifa na haki isiyoweza kuondolewa ya watu wa Uganda na Tanzania ya kujiamulia mustakabali wao na mamlaka ya kujitawala, nchi za Kiafrika ni huru, tunakaribisha ushauri wowote mzuri lakini hatutokubali kupokea maagizo na amri kutoka kwa wadau kutoka nje,”amesema Mchinjita.

Amesema ACT-Wazalendo kinasikitishwa na azimio hilo la Septemba 15, mwaka huu lililodai mradi huo utaharibu bayoanuai (viumbehai) na kusababisha mabadiliko ya tabianchi, kitu ambacho siyo kweli.

Kwa mujibu wa Mchinjita, madai hayo ya Bunge la EU yanalenga kuzuia uanzishwaji wa kiwanda cha kusafisha mafuta na kutoa shinikizo kwa wawekezaji watarajiwa kusitisha uamuzi wa mwisho wa kuwekeza mradi huo.

Amesema chama chao kinatambua na kuthamini hatua na juhudi zinazofanywa na wanaharakati wa mazingira, watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia (Azaki) za ndani ya nchi zote mbili kuzitahadharisha na kuziwajibisha serikali mbili za Uganda na Tanzania kuzingatia athari za mazingira na kujali haki za binadamu.

Pia kutokana na azimio hilo, ACT-Wazalendo kimelitaka Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoa azimio la kulinda uhuru wa Tanzania na Uganda katika kujiamulia mambo yao na kutaka mazungumzo na Bunge la Ulaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news