JAPAN KUNUNUA KILO MILIONI 30 ZA TUMBAKU TANZANIA

NA MWANDISHI WETU 

KAMPUNI ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kwa wakulima wa Tanzania katika msimu ujao wa kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatatu, Septemba 26, 2022 na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Bw. Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea ofisi zao ili kuwahakikishia utekelezaji wa mazungumzo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa TICAD 8, jijini Tunis, Agosti, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.
“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la tumbaku Tanzania,” amesema.

“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa sana. Nikiwa ziarani Tabora, nilikutana na viongozi wakuu wa vyama vya wakulima wa zao hili, na waliomba kupewa fursa ya kuongeza soko, kwa hiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” amesisitiza.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Bw. Takashi Araki.

Waziri Mkuu yuko Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe yanayotarajia kufanyika kesho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news