WAZIRI MKUU AWASILISHA SALAMU ZA RAIS SAMIA NCHINI JAPAN

NA MWANDISHI WETU 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida na kuwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kifo cha Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, wakati walipokutana kwenye kasri la Kifalme ambalo hutumika kufanyia shughuli za Kiserikali la Akasaka (Akasaka Palace), jijini Tokyo, Japan.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Akiwasilisha salamu hizo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatoa pole nyingi kwako, kwa familia ya wafiwa na kwa wananchi wa Japan kutokana na msiba huo.”

Katika mazungumzo yao, mbali na kutoa pole, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza uwepo wa mahusiano mazuri baina ya Tanzania na Japan na kumuahidi nia thabiti ya Serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Vilevile, Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kukumbushia masuala ambayo walijadiliana kwa njia ya mitandao wakati akiwa Tunisia kwenye mkutano wa TICAD 8 hasa utekelezaji wa miradi ya zamani ambayo Tanzania iliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 7 inayohusisha ujenzi wa bandari ya Kigoma, mradi wa maji wa Zanzibar na ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi Holili mkoani Kilimanjaro.
“Nimemshukuru Waziri Mkuu wa Japan kwa ahadi yake kuwa wanafuatilia pia maombi ya miradi minane ambayo tuliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 8 na majadiliano yameanza huko nyumbani.”

Miradi hiyo ni ya ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, mradi wa kusambaza maji Lugoda (Mufindi), kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete na ujenzi wa njia ya umeme ya Somanga-Fungu-Mkuranga.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amesema watatekeleza ahadi yao ya kuzisaidia nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ili zijitegemee kwa chakula. “Amesema kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) watatoa dola za Marekani milioni 300 ili kuzisaidia nchi za Afrika zizalishe chakula kwa wingi na kukabiliana na upungufu wa chakula uliojitokeza baada ya kuzuka kwa vita baina ya Urusi na Ukraine.”

“Kwenye elimu, nimemuomba Waziri Mkuu Kishida aangalie uwezekano wa vijana wetu wa digrii ya kwanza waweze kupata fursa ya kuja Japan kusomea fani za udaktari, ICT, kwani hivi sasa wanachukua wanafunzi wa Master’s na PhD tu. Tunahitaji wanaosomea digrii nao wapate fursa kama hiyo,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kesho Jumanne, Septemba 27, 2022 Waziri Mkuu atashiriki maziko ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe kwa kutoa heshima za mwisho kwenye ukumbi wa Nippon Budokan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news