Kisa cha kusisimua kutoka Mji wa Serikali Mtumba

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU moja nilipanda bodaboda ikanipeleka Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Tukianza safari hiyo katika bango linatambulisha eneo hilo kwa sasa kuna barabara nzuri sana inayokaribia kukamilika.
Nikimwambia kijana huyu sasa mambo ni safi naona nyoka amenyooka sana, kijana huyu akisema kaka hali siyo nzuri maana ajali ni nyingi sana, kwa mfano hii barabara ya kwenda Morogoro ajali kila mara na jana kuna kijana mmoja amefariki kwa kugongwa na lori.

Nilimpa pole kwa msiba huo kijana huyu akiniambia kuwa shida ya Barabara ya Morogoro siyo pana magari mawili au matatu hayawezi kwenda pamoja kwa hiyo inapaswa kupanuliwa mapema sana ili kupunguza ajali hizo kwa maana vijana wengi wa bodaboda wanagongwa wakiwa katika Service Road.

Tukiwa njiani mara tukapigiwa honi pipiiiii na kuvukwa na gari moja kama V8 iliyokuwa ikikimbikizwa kwa kasi mno. Siye hatukuwa na haraka mwendo wetu wa kobe wao mbele na sisi nyuma. Baada mwendo kidogo hii V8 ikaingia katika wizara moja na kutuacha sisi tukiendelea na safari yetu.

Kijana huyu akasema jamaa wanaendesha kwa spidi kali kumbe walikuwa wanaishia hapa? Nikajibu labda wanawahi kikaoni, akasema hawana lolote, kama kweli wao wanafanya mambo yao kwa kasi basi jengo lao nalo wajenge kwa spidi kama V8 yao.
 
“Wameanza kulijenga tangu mwezi wa 11 mwaka jana linawashinda, spidi hizo wazihamishie katika ujenzi wa jengo hilo.” Binafsi nikashituka kidogo nikasema huyu kijana mbona unaulewa mkubwa? Nikamuuliza kwani kuna majengo yanayojengwa kwa kasi zaidi ya mengine?

Akaniambia mzee, nyinyi Dodoma wageni, lakini sisi haya maeneo yalikuwa mashamba yetu na humu yapo makaburi ya mababu zetu hayakuwa yanatambuliwa tu wamelala katika ardhi hii na kila linalofanyika humu tunalifahamu vizuri sana.
 
 “Hapa yapo majengo matatu yanajengwa kwa kasi na spidi yake ni nzuri na yatakuwa ya kwanza kumalizika.”
 
Nikamuuliza majengo ya wizara gani? Akanijibu angalie hili ni jengo la wizara ya Maliasili na akaniambia angalia hilo la Wizara ya Maji na lingine kule mbele nitakuonesha.

“Yote haya yanajengwa na Wachina, hawa jamaa wana vifaa vya kutosha zege linachanganwa na mashine, linapandishwa ghorofani na mashine na kumiminiwa na mashine sasa utashindana na wewe unaechanganya na mikono, unabeba kichwani kwa karai na unamimina kwa mikono?”

Nikasema alaa kumbe akajibu ndiyo hivyo. Wenzako wanajenga saa 24 wewe unajenga saa 7 hadi 8 kwa siku unaweza kushindana naye? Nikamuuliza kwani hawa Wachina wanajenga saa 24? Kijana huyu alijibu ndiyo mwendo wa ujenzi usiku na mchana.

Mara nikafika pahala pa kushuka, nikashuka na kijana huyu akasema unaliona lile ghorofa la Wizara ya Elimu? Pale kazi yao inakwenda kwa kasi mno na ujenzi ulianza kwa kuchelewa mwezi wa Februari 2022 lakini jengo lao linalingana na majengo yaliyoanza ujenzi Novemba 2021. Siri ya mafanikio ya Mchina ni tatu kwanza vifaa bora, kujenga usiku na mchana na tatu wanawalipa vibarua wao kwa wakati.

Akasema mzee hata hapo unapoingia, msomeni Mchina anavyochanganya kokoto na mashine? Anavyobeba zege na mashine na anavyomimina zege kwa mashine? Kama hilo la Mchina Mashine Mara Tatu ni gumu basi hata kufanya kazi na saa 24 tumeshindwa? Tunawaona kila siku na mabegi yenu ya kompyuta mpakato migongoni huku mkitaka kutugonga na magari yenu jamani watoto wetu bado wadogo, mtuvumilie vumulie jamani.

“Mimi nimesoma hadi kidato cha nne nikapata zero lakini akili yangu ipo vizuri sana Mchina nimeshamsoma kitambo sana.” Nikasema hii ofisi ninayoingia nayo ipo katika tatu? Akacheka sana, hii ni Wizara ya Elimu? Akacheka sana, nikamwambia nitakunyima dili la kunibeba, akasema mzee usifanye hivyo, lakini msome Mchina, nikampa shlingi 2000/- yake na kuondoka zake. Nikilikumbuka neno lake la Mchina Mashine Mara Tatu

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments