Lusajo, Pluijm na Hassan Simba watwaa tuzo za TFF

NA GODFREY NNKO

MSHAMBULIAJI wa Namungo FC, Relliant Lusajo ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa mwezi Agosti, huku Mholanzi, Hans van der Pluijm wa Singida Big Stars akiibuka kocha bora wa mwezi.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 10, 2022 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao cha kamati ya tuzo za TFF kilichokutana jijini Dar es Salaam wiki hii kilimchagua Lusajo baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa mwezi Agosti ambapo kila timu ilicheza michezo miwili, akiisaidia Namungo FC kupata alama nne, ikishinda mchezo mmoja na sare moja, huku yeye akifunga mabao matatu.

"Nyota huyo aliwashinda Tepsie Evans wa Azam FC na Fiston Mayele wa Yanga SC zote za Dar es Salaam,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa, Pluijm aliwashinda Zoran Maki wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga, ambapo kwa mwezi huo Singida iliifnga Tanzania Prisons bao 1-0, pia ikafunga Mbeya City mabao 2-1.

"Pia, Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Liti mkoani Singida, Hassan Simba kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Agosti, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani,"imeongeza taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments