Mgombea CCM aondolewa kwenye kinyang’anyiro kwa kupigiwa simu, Kinana atoa neno

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ameshangazwa na taarifa za Nuru Magege (pichani) kuondolewa kwenye orodha wa wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini, Pwani kwa njia ya simu akisema huo sio utaratibu wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambazwa katika mitandao jioni hii, Nuru Magege ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo Wilaya Kibaha Mjini ameondolewa kwenye kinyang’anyiro kwa kupigiwa simu.

“Ni kweli nimepigiwa simu jina langu limeondolewa,” alisema Magege huku akidai hajui sababu. Magege hakutaka kuzungumza zaidi.

Wiki iliyopita jina la Magege pia liliondolewa katika orodha ya wagombea, lakini CCM makao makuu baada ya kufuatilia hawakuona sababu ya kulikata jina lake, walimpa barua ya kumruhusu kuendelea kutetea nafasi yake.

Uchaguzi uliopangwa kufanywa ulilazimika kusogezwa mbele kutokana na sintofahamu hiyo. Uchaguzi sasa unatarajiwa kufanyika Ijumaa tarehe 30 Septemba katika Ukumbi wa Triple J, Picha ya Ndege Kibaha mjini, huku jina la Magege pia likiondolewa.

Baadhi ya wana CCM wameonekana kukerwa na tukio hilo huku wengine wakisema kinachonekana kuna mipango ya kupanga safu ya uongozi na kuomba viongozi wa juu CCM kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu.

“Huyu ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya Wazazi wilaya, kwanini ukate jina lake?,” anahoji mwanachama mmoja na kusema “inaonekana ni kama kuna mtu mwenye nguvu za fedha ndiye anayeiendesha Kibaha, wamezibwa midomo hadi tuliokuwa tunawaamini kwa kupigania haki ndani ya chama, hili ni jambo baya sana”.

Mwingine anaongeza “Taarifa zote juu ya mambo ya hovyo yaliyofanyika juu ya chaguzi ya wazazi ninazo mpaka zinatia aibu kichama kibaha. Leo jina linarudi kwa barua, kesho linaondolewa simu”.

Baadhi ya wanachama wanapendekeza chama kiunde kamati maalum kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakidai kuna viashiria tata; simu za baadhi ya viongozi zifuatiliwe ili kujua ukweli wa sakata hili.

Baadhi ya viongozi wa wilaya, mkoa na Taifa wa chama na jumuiya walipopigiwa simu kwa nyakati tofauti walionyesha kushangazwa na kitendo hicho huku baadhi yao wakisema kuna agizo limetoka juu la kumzuia Magege kugombea.

"Chama sio mtu, chama ni vikao, kama Magege ana makosa vikao ndio vilipaswa kukaa, na hata kama ni vikao vipo vya kuonya na kuelekeza. Kuna tatizo hapa," alisema kiongozi mmoja mkubwa ngazi ya Taifa Jumuiya ya Wazazi. Hata hivyo,Makamu Mwenyekiti ameahidi kulifuatilia suala hilo.

Post a Comment

0 Comments