Ni jukumu letu sote kuwatunza wazee-Dkt.Shein

NA DIRAMAKINI

RAIS mstaafu wa Awamu ya Saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt.Ali Mohamed Shein amesema suala la kuwatunza wazee ni jukumu la pande zote hivyo halikwepeki.

Mheshimiwa Dkt.Shein ameyasema hayo Septemba 29, 2022 jijini Dodoma wakati akifungua mjadala kuhusu wazee unaoendeshwa na Shirika la HelpAge na Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Huku Oktoba Mosi ya kila mwaka huwa ni siku ya wazee Duniani.

Amesema, ni wakati wa Serikali na wanajamii kuungana pamoja kuwasaidia wazee kwa kuwa bila wao nchi isingekuwa mahali pazuri kama ilivyo kwa sasa.

"Ni lazima tuwatambue wazee kuwa wana umuhimu mkubwa, lazima tukubali kwamba jukumu la kuwalea ni letu sote bila kukwepa,"amesema Rais mstaafu Dkt.Shein.

Mwaka 2019

Akiwa madarakani, mwezi Agosti 2019, Mheshimiwa Dkt.Shein aliitaka jamii kuzingatia umuhimu wa kuwaheshuimu na kuwatendea wema wazee, kwa kutambuwa kuwa ni misingi muhimu ya silka, malezi na utamaduni wa Wazanzibari.

Rais mstaafu Dkt.Ali Mohamed Shein.

Dkt. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazee na Wastaafu Zanzibar (JUWAZA), uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdul wakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.

Alisema, jamii imekumbwa na vitendo vya udhalilishaji na unyanyapaa dhidi ya wazee, huku kukiwa na watu ndani ya familia wanaowadharau wazee wao kwa kuwatukana pamoja na kuwahusisha na imani za kishirikina na dhana za kuhusika na vitendo viovu, ikiwemo uchawi na wanga.

Dkt.Shein alisema, kuna baadhi ya vijana mbali na kusomeshwa vyema na wazee wao, wamekuwa wakiwadharau wazee kwa kigezo kuwa hawaendani na hadhi walizonazo, mambo yanayochangia na kuwafanya wazee kukosa amani, matunzo, misaada na haki wanazostahiki.

“Haki ya kuheshimiwa na kutunzwa ni ya msingi kwa kila mzee, vijana wana wajibu wa kuwapa wazee wao haki zao kwani huo ni wajibu wao,”Mheshimiwa Dkt.Shein alisema kipindi hicho wakati akizungumza na wazee hao.

Pia aliitaka jamii kuendelea kuwaheshimu wazee kutokana na mambo mbalimbali makubwa waliyolifanyia Taifa na kusisistiza haja ya kuendelea kuwatunza an kuwaenzi ili kupata fursa ya kuchota hekima na busara kutoka kwao.

Alisema, nchi zote zinazoendelea zimekuwa na utamaduni wa kuwaenzi na kuwathamni wazee na wastaafu na kuwatumia ipasavyo, hususani pale kunapohitajika ushauri wa mambo mbalimbali, kutokana ana maarifa, hekima na uzoefu wao katika masuala ya kimaisha.

Aidha, alisema ni muhimu kuzingatia suala la kuwatunza wazee kuwa limetiliwa mkazo katika mafunzo ya Dini zote, ikiwa ni hatua maalum katika kuwatendea wema.

Dkt.Shein alisema katika kudhihirisha dhamira njema ya Serikali katika kuyashughulikia masuala ya wazee, mara baada ya Mapinduzi matukufu ya 1964, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume alianzisha ujenzi wa nyumba za wazee kwa lengo la kuwahifadhi, hususan wale waliokosa uwezo na watu wa kuwahudumia.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiendeleza utaratibu wa kuwapa hifadhi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee, kwa kutambuwa kuwa huo ni wajibu wake wa msingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news