Mwanahabari Dismas Lyassa ajitosa kuwania Uenezi CCM mkoani Pwani

NA DIRAMAKINI

MWANDISHI wa habari na mjasiriamali,Bw.Dismas Lyassa (pichani kulia) amejitokeza kugombea Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Pwani huku akiahidi kushirikiana na wanachama na viongozi wengine kuleta mabadiliko katika mkoa huo.

Akizungumza hivi karibuni baada ya kurudisha fomu, Lyassa ambaye amekuwa mhariri katika vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwemo kumiliki gazeti lake binafsi alilolipa jina la Jiamini, anasema ameipitia katiba na kuisoma vizuri na kuona anazo sifa zinazostahiki na kumruhusu kugombea.

"Mojawapo ya eneo katika katiba inasema Mwenezi anapaswa kuwa na mawasiliano na vyombo vya habari na waandishi wa habari, mimi nimekuwa mwandishi na mhariri wa muda mrefu, nina mtandao mzuri kwa maana ya mawasiliano na waandishi wenzangu," anasema Lyassa.

Lyassa anaongeza kuwa, "Ahadi yangu kuu ni moja...kufanya kazi kwa mujibu wa maagizo ya katiba ya chama na maelekezo ya viongozi wangu pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa wanachama wengine juu ya namna bora ya kuendelea kuimarisha mawasiliano katika chama chetu..nitahakikisha kunakuwa na mafunzo kwa wenezi wote kuanzia mabalozi, matawi hadi wilaya zote kuhusu masuala ya uenezi, kuhakikisha suala la kadi za kidigitali linaendeshwa kwa kasi, nitafanya ziara za mara kwa mara kuanzia ngazi za matawi, kata na wilaya ili kuhakikisha changamoto zozote zinazojitokeza zinashughulikiwa haraka ikiwamo kukaa na viongozi wa Serikali ngazi za matawi, kata na wilaya ili waweze kuendelea kutekeleza ipasavyo ilani ya chama".

Lyassa anasisitiza " nje ya kufanya kazi kama Mhariri na meneja wa masuala ya habari, nimekuwa pia kama Meneja wa Mawasiliano na Masoko katika mashirika na taasisi tofauti, nitatumia ujuzi na uzoefu huo kushirikiana na wenzangu kukipeleka mbele chama chetu".

Dismas Lyassa ambaye kichama kwa sasa ni mwenyekiti wa CCM Tawi nafasi aliyogombea baada ya kuombwa na wazee kuigombea, nje ya kusomea uandishi wa habari ana Stashahada ya Uzamiliki katika Uongozi na Utawala kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma aliyohitimu mwaka 2014. Aliwahi kugombea Ubunge wa Afrika Mashariki 2016, Ubunge Jimbo la Mlimba Morogoro mwaka 2015.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news