MFANYE MAMBO MAKUBWA:Simba na Yanga SC hongera, mko hatua nyingine

NA LWAGA MWAMBANDE

SIMBA SC inakwenda kuchuana na Primiero do Agosto ya Angola katika raundi ya mwisho ya kuwania kucheza Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku watani zao Yanga SC watakwenda kumenyana na Al-Hilal FC ya Omdurman nchini Sudan.

Hatua hii inatokana na ushindi mnono ambao klabu hizo mbili zimeupata katika mechi kwa nyakati tofauti baina ya Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi iliyokung'utwa mabao manne na Simba SC huku Zalan FC ya Sudan Kusini wakifurumishwa kwa mabao tisa na Yanga SC katika Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasema, huu ni ushindi na heshima tosha kwa Watanzania, ambao wanaendelea kuziombea klabu hizo ili ziweze kufanya vyema katika anga la Kimataifa ikizingatiwa kuwa, ushindi na matokeo bora si sifa kwao tu, bali ni ushindi wa Taifa. Ungana naye hapa chini aweze kukushirikisha jambo kupitia shairi lifuatalo;


1:Simba na Yanga hongera, mko hatua nyingine,
Pia Kipanga hongera, mmefanya kivingine,
Wengine wametukera, tungelikuwa wanene,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

2:Kwenye Ubingwa Afrika, hii hatua nyingine,
Ugumu waongezeka, Yanga Simba muuone,
Muhimu kuimarika, mkienda mpambane,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

3:Matarajio makubwa, timu zetu hizi nne,
Mfanye mambo makubwa, Afrika pande nne,
Zile dola za ubwabwa, tuzipate tuzione,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

4:Hapa kwetu Tanzania, zasalia timu nne,
Kule Kipanga kwa nia, tutazidi tuione,
Huku Bara Tanzania, ni tatu kati ya nne,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

4:Geita Gold butu, na ile timu nyingine,
Hazijasogea katu, na zingine zifanane,
Sikate tamaa katu, jaribu mwaka mwingine,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

5:Azam inaungana, zilizosalia nne,
Mbele kwenda kupambana, ili jasho zitoane,
Lengo tuzidi ziona, kwenye raundi zingine,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

6:Pongezi kwa wachezaji, zifike na wazione,
Walimu wenye kipaji, keki nao watafune,
Na wote wawekezaji, watambe na wajivune,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

7:Wito timu Tanzania, basi na tusirogane,
Uchawi kusaidia, timu za nchi zingine,
Bora kuwanyamazia, wenyewe wakapambane,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

8:Timu zinapoinuka, fahari sote tuone,
Sote tunanufaika, mwaka jana tuuone,
Simba na nyavu kucheka, tulipata timu nne,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

9:Heko pia Serikali, furaha yetu muone,
Hamasa yenu aghali, ni nzuri kama senene,
Hamjanyamaza tuli, mwahimiza tupambane,
Sasa hatua nyingine, soka bara Afrika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news