Rais Dkt.Mwinyi aishirikisha China hitaji muhimu katika Sekta ya Afya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimwa Dkt.Hussein Mwinyi ameiomba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kuangalia uwezekano wa kutuma Madaktari Bingwa katika nyanja mbalimbali ili kwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya kupitia hospitali za wilaya zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimvisha nishani mmoja wa Madaktari Bingwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China, wanaomaliza muda wao wa kazi Zanzibar wa kutoa huduma za matibabu katika Hospitali za Unguja na Pemba walipofika Ikulu jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kumuaga. (PICHA NA IKULU).

Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Septemba 10, 2022 Ikulu jijini Zanzibar katika hafla ya kuwaaga madaktari 21 kutoka China, ambao walikuwepo nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoa huduma katika hospitali mbalimbali za Unguja na Pemba.

Amesema, wakati huu Serikali ikikamilisha ujenzi wa hospitali za wilaya katika wilaya 11 za Unguja na Pemba, Hospitali ya Mkoa pamoja na Hospitali ya Rufaa Binguni, kuna umuhimu wa China kutuma madaktari bingwa katika nyanja mbalimbali, kupitia utaratibu huo wa kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya hospitali hizo ili kuondokana na changamoto ya kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Amesema, hospitali hizo za wilaya, Mkoa na Hospitali ya Rufaa pale zitakapokamilika zitakuwa na vifaa na maeneo yote muhimu katika utoaji wa huduma, hivyo timu ijayo ya madaktari kutoka China itakuwa katika mazingira bora ya kufanya kazi.
Dkt.Mwinyi aliipongeza Timu hiyo ya Madaktari wa Kichina kwa kazi kubwa waliyofanya wakiwa hapa nchini kwa kusaidia utoaji wa huduma za kinga, tiba, dawa pamoja na vifaa, sambamba na kufanya upasuaji wa magonjwa mbali mbali.

Aidha, aliwashukuru madaktari hao kwa kutoa mafunzo, pamoja na kuwajengea uzoefu madaktari wazalendo, wauguzi na wafanyakazi wa Sekta ya Afya.

Naye Waziri wa Afya, Ahmeid Nassor alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Amesema, tangu mwaka 1964 kumekuwepo utaratibu kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutuma timu ya madaktari hapa nchini kila mwaka, na akatumia fursa hiyo kuipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutoa huduma bora katika jamii.

Amesema, wakati wakiwa nchini, timu hiyo ilifanya kazi mbalimbali ikiwemo za upasuaji, kutoa ushauri pamoja na kutoa huduma za afya katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Abdalla Mzee, Kivunge, Mkaunduchi na Chakechake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Tuzo Maalum na Kiongozi wa Madaktari Bingwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China, Dkt. Qu, iliyotolewa na Timu ya Madaktabi Bingwa wa China, walipofia Ikulu jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wao wa kazi Zanzibar katika hospitali za Unguja na Pemba.

“Timu hiyo haikuishia kufanya kazi katika hopitali kubwa pekee bali ilifika hadi katika vituo vya afya vilivyopo vijijini, hatua hii ilibainisha ari kubwa waliyonayo madaktari hawa katika utendaji wao wa kazi uliotukuka,”alisema.

Alisema, utendaji wao umeacha athari kubwa hapa nchini na utasaidia kuwajengea uzoefu madaktari wazalendo.
Mapema, kwa niaba ya timu hiyo ya madaktari kutoka China, Dkt. Son (Machano) alisema utaratibu wa China kutuma madaktari hapa nchini uliasisiwa tangu mwaka 1964 kwa lengo la kujenga mashirkiano katika utatuzi wa changamoto za huduma za afya, ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano kati ya China na Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt.Marijani Msafiri Marijani alisema timu hiyo ya madaktari kutoka China wakati ikiwa nchini mbali na kutoa huduma katika hospitali kubwa, pia ilipata fursa ya kufika maeneo ya vijijini na kutoa huduma za uchunguzi wa maradhi mbalimbali.

Huu ni mkupuo wa 31 kwa Timu ya Madaktari kutoka China kuja Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma za afya, hii ikiwa ni timu ya 21, ambapo imehusisha madaktari katika fani mbalimbali wakiwemo madaktari wa magonjwa ya pua, koo na masikio,meno pamoja na macho
Aidha, katika timu hiyo pia kulikuwa na madaktari wa njia ya mkojo, maradhi ya akinamama, mfumo wa njia ya chakula, moyo,dawa za usingizi pamoja na mishipa ya fahamu.

Katika hafla hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi alikabidhi Medali, Vyeti na zawadi kwa madaktari hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news