Rais Dkt.Mwinyi ataja faida za mabadiliko Sheria ya Makadhi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, ana matumaini makubwa kuwa mabadiliko ya Sheria ya Makadhi yanayofanyika yataondoa utata pamoja na migongano ya kiutendaji katika mhimili wa Mahakama hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Kamati ya Sheria Mpya ya Makadhi Zanzibar, walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo Septemba 12, 2022 na kulia kwa Rais ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi na kupokea taarifa ya mwelekeo wa rasimu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Wakili Mwandamizi wa Serikali, Saleh Mbaraka.

Amesema, kutokana na dhamira njema iliyopo, ana imani kubwa kuwa sheria ijayo ya Makadhi itakuwa nzuri, yenye tija, isiyo na mivutano na yenye mwelekeo wa kujenga.

Amesema, pale rasimu hiyo itakapofikishwa katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi,wajumbe wa baraza hilo watapata fursa ya kuipitia, sambamba na Kamati ya Sheria ya Baraza hilo kushauri juu ya vipengele vinavyofaa kuingizwa au kupunguzwa.

Dkt.Mwinyi aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa dhamira ya kuja na sheria mpya ya Makadhi kutokana na mahitaji yaliyopo, akibainisha hatua ya kuwashirikisha wadau itawezesha kupata mchango wa maoni ya kutosha.

Naye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla pamoja na mambo mengine alisema kuongoza mhimili wa Mahakama, ambamo ndani yake kuna Kadhi Mkuu, kunahitajika busara kubwa.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi Wakili Mwandamizi Saleh Mbaraka, alisema lengo la sheria hiyo ni kuongeza wigo wa kutafuta haki ndani ya Mahakama za Kadhi pamoja na kuleta uharaka katika maamuzi ya kesi.
Amesema, sheria hiyo inalenga kurejesha dhana ya kuwatambua masheikh wabobezi, pamoja na kuwa na utaratibu wa kuweka hati mbalimbali na kuweza kutumika katika Mahakama mbalimbali duniani.

Aidha, alisema itatoa msukumo katika hati mbalimbali (ikiwemo za ndoa) kuweza kukubalika katika mataifa mbalimbali.

Wakili Mbaraka alieleza kuwa, kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi katika kuwasomesha Masheikh katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Saud Arabia, kupitia fedha za Serikali au za wahisani, lakini matokeo yake pale masheikh hao wanaporejea nchini huachwa bila kutumika.

Amesema kupitia sheria hiyo Masheikh hao watatambuliwa ili waweze kutoa mchango wao na kubainisha hatua hiyo itatoa ajira kwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news