Rais Dkt.Mwinyi:Serikali itashirikiana kikamilifu na TAEC

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itashirikiana kikamilifu na Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ili kuweza kukamilisha vyema majukumu yake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Bodi ya Tume ya Nguvu ya Atomiki Tanzania (TAEC), Prof.Lazaro Simon Petro (wa pili kushoto) alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo. (Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na ujumbe kutoka Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, uliofika kwa ajili ya kuelezea utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya, itahakikisha tume hiyo inatekeleza kikamilifu majukumu yake hapa Zanzibar na akatumia fursa hiyo kuipongeza kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya.

Akigusia baadhi ya mafanikio na changamoto yanayoikabii TAEC katika utekelezaji wa majukumu yake, Dkt.Mwinyi ameipongeza kwa kuwa na uharaka katika utoaji wa vibali, ikilinganishwa na taasisi nyingine za Muungano, huku akibainisha kuwepo kwa urasimu katika taasisi nyingi za Serikali.

Aidha, ameishukuru TAEC kwa udhibiti mzuri wa mionzi na kusema ni suala muhimu sana kwa afya ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa msukumo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuona masuala mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti na upungufu wa wafanyakazi unaokabili taasisi hiyo hapa Zanzibar yanapatiwa ufumbuzi.

Alieleza kuwa, Serikali itafuatilia kuhakikisha eneo la mradi wa ujenzi wa majengo ya TAEC katika eneo la Dunga Duze, Wilaya Kati Unguja linaongezwa ili kukidhi mahitaji ya taasisi hiyo.

Aidha, alisema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi itaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za tozo la ada ya kiwanja ya shilingi milioni 2.5 kwa mwaka, pamoja na kuahidi kusaidia ujenzi wa barabara ya ndani yenye urefu wa kilomita 2.5 inayotoka barabara kuu hadi eneo la mradi, akibainisha hatua hiyo itabadili mazingira ya eneo hilo.

Naye, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui aliipongeza bodi hiyo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake hapa Zanzibar, hususani katika suala la uingizaji wa bidhaa kutoka Tanzania Bara, kwa kutambua kuwa Zanzibar ni sehemu ya Muungano, tofauti ilivyo kwa taasisi nyingine za Muungano.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof.Lazaro Simon Petro amesema, TAEC inaendelea na mradi mkubwa wa ujenzi wa majengo mbalimbali hapa Zanzibar katika eneo la Dunga Zuze, unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 3.03.

Amesema, ujenzi huo utakaohusisha maabara mbalimbali umefikia kiwango cha asilimia 35 hivi sasa, ukifanyia katika eneo la ardhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,314 na kuishukuru Serikali kwa kuipatia bodi eneo hilo, ingawa bado haitoshelezi mahitaji.

Amesema, TAEC imepata mafanikio makubwa katika masuala mbalimbali hapa Zanzibar, ikiwemo utoaji wa vibali, ambapo kabla ilikuwa vikitolewa baada ya siku saba na hivi sasa hutolewa ndani ya siku moja.

Aidha, Mkurugenzi huyo akatumia fursa hiyo kuipongeza TAEC kwa kufanikiwa kutokomeza Mbung’o katika mradi uliofanyika hapa Zanzibar mwaka 1995.

Amesema, miongoni mwa changamoto inazoikabili TAEC ni uhaba wa wafanyakazi, ambapo kwa wastani wanahitajika wafanyakazi 20 na hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Serikali kibali cha kuajiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news