Rais Dkt.Mwinyi ateta na madaktari bingwa wa moyo kutoka Israel

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ujio wa madaktari kutoka Jumuiya isiyo ya Kiserikali ya ‘Save a Child’s Heart’ ya nchini Israel unaisaidia sana Serikali kuondokana na gharama kubwa ya matibabu ya ugonjwa wa moyo unaowakabili watoto hapa nchini.
Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na timu ya Madaktari wa Upasuaji wa magonjwa ya moyo kutoka Israel, ulioongozwa na Mkurugenzi wa Jumuiya hiyo Tamar Shapira.

Amesema, hatua ya madaktari hao ya kuja nchini kila mwaka na kuwachunguza watoto wanaotatizwa na ugonjwa wa moyo na hatimaye kusafirishwa hadi Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji, imeisadia sana Serikali kuondokana na gharama kubwa ya matibabu ya wagonjwa hao.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru madaktari hao kwa kushirikiana na Serikali na kufanya kazi kubwa wanayofanya ya kunusuru maisha ya watoto wa Zanzibar wanaokabiliwa na ugonjwa wa moyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Madaktari Bingwa wa Upasuaji kutoka nchini Israel wakiongozwa na Mkurugenzi wa Save a Child’s Heart, Bi. Tamar Shapira,walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo. (Picha na Ikulu).

Amesema, Serikali haina uwezo wa kutosha wa kuwahudumia watoto wote wanaokabiliwa na changamoto ya ugonjwa huo kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo hilo linalowakabili watoto wengi.

Aidha, amesema mradi unaolengwa kutekelezwa wa ujenzi wa kitengo cha matibabu ya moyo kwa watoto, utasaidia juhudi za Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuzingatia kuwa hatua hiyo utatoa fursa kwa wataalamu kutoka nje kuja kufanya operesheni ndogo ndogo pamoja na kuwajengea uwezo watendaji.

Aliiomba jumuiya hiyo kusaidia upatikanaji wa taaluma kwa madaktari ili hatua hiyo iende sambamba na uwepo wa kitengo hicho pale kitakapokamilia.

Naye Mkurugenzi wa Jumuiya ya ‘Save a Child’s Heart’ Tamar Shapira aliahidi jumuiya hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuhakikisha inakabiliana na tatizo la ugonjwa wa moyo linalowakabili watoto wa Zanzibar.
Mkurugenzi huyo amepongeza ushirikiano mkubwa waliopata kutoka Uongozi wa Wizara ya Afya katika kipindi chote wakiwa nchini na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliowasilishwa kwao.

Mapema, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui alisema Madaktari wa jumuiya hiyo wamekuwa na utaratibu wa kuja nchini kila mwaka na kushirikiana na Wizara Afya kwa ajili ya kuwachunguza watoto wanaokabiliwa na ugonjwa wa moyo, kufuatilia maendeleo yao pamoja na kuwafanyia upasuaji.

Amesema, Wizara Afya kwa kushirikiana na Serikali ya Norway ina azma ya kujenga Kitengo cha Matibabu ya moyo, katika jengo litakalokuwa na mahitaji yote muhimu ikiwemo vifaa, ikiwa ni hatua ya kuyahami maisha ya watoto wa Zanzibar wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Madaktari wa Upasuaji kutoka Jumuiya ya ‘Save a Child’s Heart’ wamekuwa na utaratibu wa kuja nchini kila mwaka kwa ajili ya kuwachunguza watoto wanaokabiliwa na ugonjwa wa moyo, wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi 17, ambapo tangu utaratibu huo kuanza mnamo mwaka 1999, jumla ya watoto 780 wamefanyiwa upasuaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news