WAZIRI MKUU ATAKA NGUVU ZAIDI UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewçataka wadau wote wa uwezeshaji wananchi kiuchumi waongeze nguvu katika kutoa huduma za uwezeshaji hasa maeneo ya pembezoni ya miji na vijijini ili kufikia malengo ya nchi katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Ametoa wito hio leo Septemba 19, 2022 wakati akifungua kongamano la sita la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

“Pamoja na wito huo, Mikoa ambayo imeanzisha vituo vya uwezeshaji iendelee kuboresha miundombinu ili vituo hivyo vikidhi ubora na viwango katika kutoa huduma za uwezeshaji”

Amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarani Serikali imeendeleza azma yake ya kuwawezesha wananchi ikiwemo utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu.

“Katika mwaka 2021/22, Serikali kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi iliwezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya shilingi bilioni 903 kwa wanufaika wapatao milioni 5.9 nchi nzima”.

Ameongeza kuwa katika mwaka 2021/2022 jumla ya watanzania 72,395 walipata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na ushiriki wao kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local Content). “Aidha, miradi ya kimkakati ilitoa kandarasi ndogo kwa kuingia mikataba na kampuni 2,019 za Watanzania kwa huduma mbalimbali.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka taasisi za fedha, mifuko na program za uwezeshaji zihakikishe zinapunguza riba za mikopo hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja ili kukuza biashara na kuchochea uchumi.

Kadhaluka, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo ziendelee kufanya maboresho ya huduma na kuwahamasisha wananchi wa kawaida waweze kuzifikia huduma wanazozitoa. “Baadhi ya maeneo mabenki yamezungukwa na shughuli za wajasirimali lakini sehemu kubwa hawana akaunti wala hawahudumiwi na taasisi hizo.”

Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka na kuimarisha miundombinu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Ameongeza kuwa kupitia ruzuku zinazotolewa na Serikali wananchi wanapaswa kuona namna ya kuwekeza ili baadae waweze kuwasaidia Watanzania wengine kupitia faida aliyoipata. “ Tuzitumie ruzuku hizi ili kuhakikisha tunalivusha Taifa letu na kuondokana na umasikini.”

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Beng’i Issa amesema kuwa baraza hilo limefanikiwa kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi 18 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Geita, Rukwa na Kigoma.

“Vituo hivi kwa mwaka wa fedha 2021/22 vimeweza kuhudumia Watanzania 11,799, ambapo wanawake walikuwa 6,157 (52%) na wanaume 5,642 (48%) na jumla ya mikopo ya shilingi bilioni 28 imetolewa katika vituo hivyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 kutoka kwenye mikopo iliyotolewa kwa mwaka 2020/2021 na jumla ya biashara 15,860 zimeweza kurasimishwa katika vituo hivi, hii ni utekelezaji wa maelekezo uliyotoa mwaka 2018”

Kaulimbiu ya Kongamano hilo ni Uwezeshaji Wananchi katika Uwekezaji ambayo inalenga kutambua jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha sekta binafsi na kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora kwa Watanzania kuwekeza na kunufaika na uwekezaji unaofanyika nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news