Australia yaahidi mambo mazuri Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi asisitiza Uchumi wa Buluu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikano uliopo kati yake na Australia kwa maslahi ya nchi mbili hizo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Balozi wa Australia, Mhe.Luke Williams (katikati), katika nchi za Kenya,Rwanda na Tanzania,pia anawakilisha nchi yake Somalia na Burundi wakati wa mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar akiwa na ujumbe wake.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na Balozi wa Australia nchini Tanzania, Luke Williams ambaye pia anaziwakilisha nchi za Kenya, Rwanda, Somalia na Burundi, ambapo amefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, kuna umuhimu kwa nchi mbili hizo kuendeleza ushirikiano uliopo wakati huu Zanzibar ikiweka kipaumbele katika kuimarisha uchumi wake kupitia Sekta za Uchumi wa Buluu, unaohusisha sekta za utalii, kilimo cha mwani na uvuvi.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa kuiomba Australia kusaidia uimarishaji wa sekta hizo na kumpongeza Balozi huyo kwa dhamira yake ya kusaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo.

Naye Balozi wa Australia nchini Tanzania, Luke Williams aliahidi kuendeleza ushirikano uliopo kati ya Australia na Tanzania pamoja na kuunga mkono azma ya Zanzibar katika kuimarisha Sekta ya Uchumi wa Buluu kwa kuzingatia uwepo wa fursa mbalimbali.

Amesema, Zanzibar ni kituo muhimu cha utalii kutokana na historia yake, kuwa na mandhari ya kuvutia pamoja na utamaduni wa watu wake.

Alimhakikisha Rais Dkt.Mwinyi kuwa atafanya juhudi kusaidia uendelezaji wa kilimo kwa kuzingatia Zanzibar ina utajiri katika uzalishaji wa viungo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news