Rais Dkt.Mwinyi:Misikiti, madrasa yatumike kuelimisha jamii umuhimu wa malezi bora kwa watoto

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Misikiti pamoja na Madrasa zinazojengwa zinapaswa kutumika kuielimisha jamii umuhimu wa malezi bora ya watoto ili wawe na hofu ya Mungu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia hotuba ya Sala ya Ijumaa ikisomwa na Sheikh Abdulkarim Said, iliyofanyika katika Masjid Huda Masingini baada ya kuufungua Msikiti huo leo Septemba 23, 2022 na kulia kwa Rais ni Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Alhaj Haroun Ali Suleiman.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi amesema hayo, katika ufunguzi wa Msikiti mpya wa Al hudda uliopo eneo la Masingini Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja, uliojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya ‘Al-noor Cheritabla Agency for the Needy’, hafla iliyokwenda sambamba na Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema, kumekuwepo mmong’onyoko mkubwa wa maadili katika jamii hususani kwa vijana kujihusisha na vitendo viovu, ikiwemo vya udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na wizi na ubadhirifu wa mali za Serikali, mambo aliyoeleza yanapaswa kuzungumzwa na kupatiwa ufumbuzi kupitia Misikiti.

Amesema matukio hayo na mengineyo mengi yalio kinyume na maadili yamekuwa yakifanyika kwa vile jamii imekosa hofu ya Mungu, hivyo akatoa rai kwa jamii kuimarisha malezi mema kwa watoto tangu wakiwa wadogo ili waweze kukua wakiwa na hofu ya Mungu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia waumini wa Dini ya Kiislam Masingini Wilaya ya Magharibi “A”Unguja, baada ya kuufungua Msikiti huo na Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Huda leo.(Picha na Ikulu).

Katika hatua nyingine, Alhaj Dkt.Mwinyi aliutaka uongozi kusimamia utunzaji wa msikiti huo ili waumini wanaofika waweze kutekeleza ibada katika mazingira bora.

Amewapongeza wafadhili waliojenga msikiti huo pamoja na wananchi wote waliofanikisha ujenzi huo na akatumia fursa hiyo kuwashukuru kwa dhati kwa kujenga eneo la kuchezea watoto, akibainisha hatua hiyo itatoa fursa kwao ya kucheza pamoja na kujifunza.

Aidha, ameipongeza taasisi ya Al –Noor Cheritable Agency for the Needy kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuenga majengo mbalimbali ya kidini pamoja na huduma za kijamii katika ameneo mbalimbali nchini.

Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab amesema hatua ya Rais Alhaj Dk. Mwinyi ya kufungua msikiti huo ni kitendo kitukufu kilichopata kufanywa na Mtume Muhammad (SAW).

Mapema, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwataka waislamu kuuimarisha msikiti huo kwa kuunadhifisha na kuufanyia matengenezo pale unapoharibika, sambamba na kutumika kama kituo cha kupata taaluma.

Sheikh Khalid amewataka wananchi kuondokana na tabia ya kuwatupia lawama viongozi kwa mambo maovu yanayofanyika katika jamii na akatumia fursa hiyo kuitaka jamii kufanya juhudi kuyaondoa maovu hayo kwa mikono yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Ufunguo wa Masjid Huda Imamu Mkuu wa Msikiti huo Sheikh Ali Rashid Khamis, baada ya kumalizika Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti huo uliofunguliwa leo.(Picha na Ikulu).

Amesema katika zama hizi mitandao imekuwa ikitumika vibaya kubadili mitazamo ya mambo mema ili yaonekane mabaya na hayana manufaa yoyote kwa jamii, akitolea mfano suala la Utalii, ambapo ndani ya Kuraani limebainishwa kuwa na manufaa.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa ‘Al-noor Cheritable Agency for the Needy ‘ Sheikh Nadir Mahafoudh aliushukuru uongozi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) kwa kusaidia upatikanaji wa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo pamoja na ujenzi wa ukuta.

Amesema, taasisi hiyo imekubali ombi la wananchi na uongozi wa kikosi hicho cha KMKM la kujenga Kiliniki katika eneo hilo, ili kuwandolea shida ya matibabu inayowakabili.

Amesema msikiti huo una uwezo wa kuswaliwa na waumini 700 kwa wakati mmoja kupitia eneo la ndani na nje, huku wanafunzi wapatao 250 wataweza kupata fursa ya kujifunza katika madrasa hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kufungua Masjid Huda ulioko Masingini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja leo kabla ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo, kulia kwa Rais ni Mkurugenzi Mkuu wa Al Noor Charitable Agency Zanzibar,Sheikh Nadir Mahfoudh na Sheikh Luay Mohammed Mahfoudh na kushoto kwa Rais ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Alhaj Haroun Ali Suleiman.(Picha na Ikulu). 

Aidha, Katibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Abdulkarim Said alisisitiza umuhimu wa waislamu kufanya juhudi za kujenga,kuipenda na kujishughulisha na masuala mbalimbali yanayohusu misikiti, kwa kigezo cha kupata fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu..

Post a Comment

0 Comments