Rais Dkt.Mwinyi:Mkaitangaze Tanzania, kuangalia fursa mbalimbali za kiuchumi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi kufanya juhudi za kuitangaza Tanzania pamoja na kuangalia fursa za kiuchumi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wa pili kulia ni Mhe.Balozi Simon N.Siro nchini Zimbabwe, Mhe.Balozi Lt.Jen.Mathew E.Mkingule nchini Zambia na Mhe.Balozi Caroline Chipeta nchini Uholanzi walipofika Ikulu leo kujitambulisha na kupata maelekezo ya kazi watapofika katika vituo vyao vya kazi.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi ametoa wito huo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania, akiwemo Balozi Simon N. Siro (Zimbabwe), Luteni Jenerali Mathew E. Mkingule (Zambia) pamoja na Balozi Caroline Chipeta anayeiwakilisha Tanzania nchini Uholanzi, waliofika Ikulu kwa ajili ya kuagana.

Amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa Mabalozi hao kuitangaza vyema Tanzania katika nchi hizo kwa kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo pamoja na kuangalia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana, ikiwemo za uuzaji bidhaa au utoaji wa huduma.

Amesema, katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi, Serikali imeweka kipaumbele sekta za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kukuza uchumi wake, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuzifanyia kazi fursa ziliomo katika sekta hizo; ikiwemo ya Uvuvi, mafuta na Gesi asilia na nyinginezo.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kumtaka Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Caroline Chipeta kuweka nguvu ili kuongeza idadi ya watalii wa nchi hiyo wanaozuru nchini.

Amesema, kwa kipindi kirefu sasa, Zanzibar imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka nchi za Ulaya, Ulaya Mashariki pamoja na Marekani, hivyo akabainisha umuhimu wa kuelekeza nguvu zaidi katika soko la watalii kutoka nchi za Scandanavia.

Aidha, Dkt.Mwinyi amewataka mabalozi hao kuchangamkia fursa za masoko ya mazao ya karafuu na viungo kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa nchi hiyo pamoja na wale wa Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe na Zambia kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kwa kuangalia fursa za kibiashara zilizopo katika nchi hizo pamoja na kuzingatia suala la ulinzi na usalama.

Nao mabalozi hao kwa nyakati tofauti walimshukuru Rais Dkt.Mwinyi kwa maelekezo aliyowapa na wakaahidi kuyafanyia kazi ili kuleta ustawi wa Tanzania na watu wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiwa katika picha na mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wa pili kushoto ni Mhe.Balozi Simon N. Siro nchini Zimbabwe, Mhe.Balozi Lt.Jen.Mathew E.Mkingule nchini Zambia (kushoto) na Mhe.Balozi Caroline Chipeta nchini Uholanzi mara baada ya kupata maelekezo ya kazi watapofika katika vituo vyao vya kazi walipofika Ikulu leo kujitambulisha.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Simon N. Siro alisema ataangalia kwa kina fursa za kiuchumi zilizopo nchini humo, hususani katika kilimo cha zao la mahindi ili kubaini sababu za nchi hiyo kuzalisha bidhaa hiyo kwa kiwango kikubwa, sambamba na kuahidi kuangalia namna ya kuwaunganisha watalii wanaozuru nchi hiyo ili waweze kufika hadi Tanzania.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew E. Mkingule, alisema ataendeleza ushirkiano wa kihistoria uliopo kati ya Taifa hilo na Tanzania pamoja na kuangalia namna ya kuchakata mafuta yanayosafirishwa kupitia Bomba la Mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Zambia pamoja na kuangalia fursa nyingine za kibiashara kupitia Reli ya Tazara.

Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Caroline Chipeta, alisema atafanya juhudi ili kuhakikisha idadi ya watalii wanaotoka Uhalonzi kuja Tanzania inaongezeka pamoja kuongeza ushirikiano katika sekta ya biashara ili kuona kampuni nyingi zaidi kutoka nchi hiyo zinakuja nchini kufanya biashara, ikiwemo uzalishaji wa mbegu pamoja na kusafirisha maua.

Post a Comment

0 Comments