Rais Samia ataja njia za kuwakomboa kiuchumi wanawake, vijana barani Afrika

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amesema kuwa,Tanzania na Bara la Afrika wakiwekeza zaidi katika sayansi na teknolojia kwa vijana wanaweza kuwa sehemu muhimu ya kustawisha uchumi kama ilivyo kwa Taifa la China.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwenye Kongamano la Wanawake na Vijana wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) lililofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2022. (Picha na Ikulu).

Hayo ameyasema leo Septemba 12, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika ambao unawakutanisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka barani Afrika.

Pia amesema, ni muhimu wanawake na vijana wakajengewa uwezo kupitia elimu ikiwa ni pamoja na kutumia sayansi na teknolojia itakayowawezesha kumiliki na kutumia rasilimali za Afrika, kujenga na kukuza Afrika ya viwanda na biashara kwa uchumi imara.

"Tutakapokwenda kutekeleza hili, tutaangalia lengo namba mbili ambalo linaangazia biashara Afrika, ambalo linasisitiza kuhusu kuwa na raia walioelimika, wenye maarifa ambao wanaweza kwenda sambamba na kasi ya sayansi na teknolojia,"amesema.

Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, "Ninataka kutilia mkazo suala la elimu kwa vijana kuhusu sayansi na tekolojia, na mfano mzuri ni kwa nchi ya China ambayo uchumi wake kupitia sayansi na teknolojia unajengwa na vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35, unaweza kukuta maprofesa wengi wa miaka 35 ambao wamebobea katika masuala ya sayansi na teknolojia na ndiyo wanaongoza makapuni mengi yanayozalisha sana kwenye nchi yao.

"Kwa hiyo na sisi tukijielekeza huko, Afrika na Tanzania kwa ujumla tuna vijana wengi ambao wanaweza wakajenga uchumi wetu, lakini pia niungane na Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, kwamba mkutano huu utoke na mapendekezo ya kisera na mikakati madhubuti ya kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

"Niwaombe wanawake na vijana wa Afrika, kuungana nami tunapochukua hatua hii ya kihistoria kuelekea utekelezaji wa maono ya wanzilishi wetu wa Ajenda Jumuishi ya Afrika Tunayoitaka, tunapaswa kutumia eneo hilo la biashara kama jukwaa la kuendeleza uwezeshaji wa wanawake na vijana wa Afrika ikiwa ni miongoni mwa malengo muhimu ya ajenda 2063 na kuimarisha upatikanaji wa fursa za biashara kwa wanawake na vijana ili kuwaimarisha kiuchumi na kukuza uwezo wa uzalishaji wa nchi zetu,"amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

Pia Rais Samia amesema kuwa, Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa duniani, "lakini pia tunaambiwa ni bara maskini kuliko yote duniani,kupitia mkutano huu ninaomba viongozi wenzangu tuendelee kuwekeza zaidi katika rasilimali watu hususani wanawake na vijana.

"Tukiwa na nguvu kazi imara, yenye ujuzi wa kutosha tutatumia rasilimali zetu vizuri ikiwa ni pamoja na kuziongezea thamani na kuendeleza ukuaji wa uchumi, hatimaye kuwezesha Afrika kuwa na mchango mkubwa katika soko la Dunia,"amesema

Mheshimiwa Rais Samia amesema,ili kushirikisha wanawake na vijana, wawezeshwe kushiriki kikamilifu katika biashara nchi za Afrika kupitia majadiliano ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika zilikubaliana kwa kauli moja kuanzisha Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara.

"Nimefahamishwa majadiliano ya kuandaa itifaki hiyo katika biashara bado yanaendelea. Na itifaki itakapokamilika na kutekelezwa kikamilifu nina imani itatimiza ipasavyo lengo la Kifungu cha 3 (e) cha Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika kinachosema kuwa, kutangaza mazingira wezeshi na jumuishi yanayozingatia uwiano wa jinsia katika Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

"Ni matumaini yangu pia, Itifaki ya Wanawake na Vijana itajikita kuendeleza wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa,ambao ni nguvu kazi ya ujenzi wa uchumi wa Afrika,"amesema Rais Samia.

Mkutano huo wa siku tatu ambao umeanza leo hadi Septemba 14, 2022 unaongozwa na kauli mbiu isemayo Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa).
"Kauli mbiu hii ni muhimu na mwafaka sana kwa vijana na wanawake barani Afrika, niwapongeze sana kwa walioibuni.Ni ukweli usiopingika kuwa,wanawake na vijana huwekeza zaidi kwa ajili ya familia zao, lakini zaidi wanawake katika maeneo ya elimu, afya na lishe na kujenga uchumi kwa mustakabali wa jamii kwa ujumla.

"Hivyo kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi kupitia ushiriki wao katika biashara kunatengeneza fursa za uhakika za ajira, kwa kila mtu na uimara wa Taifa na jamii kwa ujumla.

"Mtakumbuka, Ajenda ya 2063 ya Afrika Tuitakayo (The Africa We Want),ndoto yake ni kuwa na Afrika iliyofanikiwa na kustawi yenye nguvu, amani na mshikamano. Hivyo, ni jukumu letu sote kuhakikisha, tunafanya mabadiliko ya kiuchumi katika bara letu ili kuleta maisha bora kwa watu wetu. Ili hayo yaweze kutokea, ni lazima kuwajengea uwezo wanawake na vijana washiriki kikamilifu katika biashara na kutumia ipasavyo, fursa zitokanazo na soko la Afrika.

Rais Samia amesema kuwa, miongoni mwa malengo ya Ajenda 2063 ya Afrika ni kuinua viwango vya maisha,kwa jamii na wananchi wote.

Amesema, katika malengo hayo, yameainisha maeneo ya vipaumbele ambavyo ni kuongeza kipato,kupunguza umaskini, njaa, kuwezesha huduma za kijamii, makazi bora na huduma nyinginezo, hivyo anaamini kupitia mkutano huo ni njia sahihi ya kutoa dira.

Rais wa Ethiopia

Awali Rais wa Shirikisho la Ethiopia, Mheshimiwa Sahle-Work Zewde amesema kwamba, mkutano huo unapaswa utoke na mapendekezo ya kisera na mikakati madhubuti ya kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mheshimiwa Zewde amesema kuwa, wanawake na vijana ni nguvu kazi kubwa ambayo ikiandaliwa mazingira wezeshi inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kustawisha uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

"Ni matarajio yetu, baada ya mkutano huo wa siku tatu, mkakuja na mapendekezo ya kisera ambayo yatatupa mwongozo ili kuyafanyia kazi,"amesema.

Dkt. Joyce Banda

Kwa upande rais mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Dkt.Joyce Hilda Banda, mkutano huo wa siku tatu umebeba dhamana kubwa wa kujadili na kuja na mapendekezo ambayo yatasaidia kuainisha zilipo fursa za kiuchumi na namna ya kuzitumia ili ziweze kuwa na matokeo mazuri kwa wanawake na vijana barani Afrika.

"Watoto wetu na mabinti zetu wamekuwa wakifia katika Bahari ya Mediterranean wanapokuwa wakielekea Ulaya kutafuta fursa za ajira na wengine wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili, hivyo umefika wakati viongozi wa kisiasa kuweka nguvu katika utashi wa kisiasa ambao utaleta majawabu juu ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo,ikizingatiwa kuwa, Afrika kuna fursa nyingi za kiuchumi,"amesema Dkt.Banda.

AfCFTA

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamikele Mene amesema kuwa, mkutano huo ni muhimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya vikao vya wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao waliazimia kupanua ushirikishwaji katika uendeshaji wa AfCFTA kupitia afua zinazosaidia vijana wa Afrika, wanawake na biashara ndogo na za kati (SMEs).
Sambamba na kuwaunganisha wafanyabiashara wasio rasmi wa mipakani katika uchumi rasmi kwa kutekeleza utaratibu wa biashara uliorasimishwa.

Amesema, sambamba na maagizo ya viongozi wa Afrika, Sekretarieti ya AfCFTA inafanya kazi ya maandalizi kuelekea katika hatua za kufanikisha Itifaki ya AfCFTA ya Wanawake na Vijana katika Biashara.

Mene amesema, itifaki hiyo inatarajiwa kushughulikia vikwazo ambavyo wanawake hukabiliana navyo wakati wa kufanya biashara barani Afrika.

Pia amesema, itaunda mazingira ambayo yataruhusu wanawake kutumia AfCFTA kupata masoko mengi, kuboresha ushindani wao, na kushiriki katika minyororo ya thamani ya kikanda.

Waziri Kijaji

Naye Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji amesema kuwa, "Ni imani yetu kwamba, wote tutatumia nafasi hii vizuri, kwa kuibua mijadala mipana itakayoleta tija kwa maendeleo ya Afrika yetu, hasa tukilenga kuwajengea uwezo wa kibiashara wanawake na vijana kwa kutoa mapendekezo ambayo yatazingatiwa katikla maandalizi ya Itifaki hiyo.

"Yenye lengo la kutatua changamoto za ushiriki wa wanawake na vijana katika biashara barani Afrika na hata dunia kwa ukubwa wake,"amesema Waziri Dkt.Kijaji.

Awali Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema,mkutano huo utajadili mada mbalimbali muhimu ikiwemo changamoto wanazokumbana nazo Wanawake na Vijana katika biashara za Mpakani (Reflecting on Challenges Women and Youth face in Cross Border Trade in Africa).

Pili ni namna ya kusaidia wanawake na vijana ambao ni kichocheo katika Sekta ya Ubunifu Barani Afrika (Supporting Women and Youth as Drivers of the Creative Industry in Africa);
Mada ya tatu ni juu ya namna ya kutumia nyenzo za kidigitali za biashara ili kuimarisha ushindani wanawake na vijana katika Soko la Eneo Huru la Afrika la Biashara (Leveraging Digital Solutions to Trade to Enhance Women’s and Youth’s Competitiveness in the AfCFTA Market).

Nne, ni namna ya kusaidia urasimishaji wa biashara za wanawake na wijana ili waweze kunufaika zaidi na Mkataba wa Eneo Huru (Women and Youth in Informal Cross Border Trade: Supporting the formalization of women and youth in trade for greater benefits under the AfCFTA).

Tano, ni majadiliano kuhusu Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Youth Roundtable on the AfCFTA Protocol on Women and Youth in Trade).

Sambamba na kuimarisha ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana katika masuala ya kifedha (Promoting Financial Inclusion for Women and Youth in Trade).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news