RAIS SAMIA AIDHINISHA BILIONI 150/- ZA RUZUKU YA MBOLEA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha shilingi bilioni 150 kutumika kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wingi na kwa gharama nafuu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, Septemba 23, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika msimu wa 2022/2023, utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kukidhi upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Ijumaa, Septemba 23, 2022 wakati akiahirisha mkutano wa nane wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Amesema Mheshimiwa Rais Samia anatambua umuhimu wa pembejeo katika kuongeza tija kwenye kilimo.

Amesema hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2022 wakulima 956,920 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku ambapo jumla ya tani 60,882 za mbolea zimenunuliwa na wakulima katika mikoa ya Arusha, Iringa, Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Ruvuma na Songwe. “Nitumie fursa hii kuilekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati.”
Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022, tathmini awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula imeonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani milioni 17.4, ambapo kati yake uzalishaji wa mazao ya nafaka ni tani milioni 9.4 na mazao yasiyo ya nafaka ni tani milioni 7.9.

“Mahitaji yote ya chakula yanayojumuisha nafaka na yasiyo ya nafaka kwa mwaka 2022/2023 ni zaidi ya tani milioni 15 ambapo tani milioni 9.5 ni za mazao ya nafaka na tani milioni 5.5 ni mazao yasiyo ya nafaka. Kwa kulinganisha uzalishaji na mahitaji, nchi yetu ina kiwango cha utoshelevu wa chakula wa asilimia 115.”

Amesema ili kuhakikisha hali ya chakula nchini inaendelea kuimarika, Serikali imeuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuhifadhi tani 147,142 na kuendelea kununua mazao ya chakula kwa ajili ya kuhifadhi. “Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuhifadhi akiba ya chakula tuliyonayo na kuwa na matumizi sahihi ya chakula.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongengezwa na wabunge baada ya kusoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, Septemba 23, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema maandalizi ya msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 yanaendelea sambamba na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo muhimu hususani mbolea.

“Wastani wa matumizi ya mbolea nchini katika kipindi cha kati ya mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 umeendelea kuwa tani 430,000. Hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2022 upatikanaji wa mbolea nchini umefikia tani 213,403 sawa na asilimia 49.6 ya wastani wa matumizi ya mbolea.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news