Serikali kumaliza upungufu wa huduma ya maji safi Mwanza

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Serikali imedhamiria kuwaondolea adha ya maji wananchi wa Jiji la Mwanza kwa kujenga miradi mikubwa ya huduma ya majisafi inayotumia chanzo cha Maji cha Ziwa Victoria.

Ameyasema hayo Septemba 14, 2022 wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Dakio jipya la Maji katika eneo la Butimba Jijini Mwanza utakaogharimu shilingi bilioni 69.

Ameelekeza mradi huo ukamilike ifikapo Noeli ya mwaka 2022, iwe zawadi ya wakazi wa jiji la Mwanza, na wananchi wanaoishi karibu na chanzo wapewe kipaumbele katika kupata huduma.

“Serikali inatambua kasi ya ukuaji wa Jiji la Mwanza pamoja na changamoto ya upatikanaji wa Majisafi katika baadhi ya maeneo ya pembezoni na yale yenye miinuko mikali, Mradi huu kwa kiasi kikubwa utaboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mengi,” Mhe. Dkt. Mpango amesema.

Amebainisha kuwa mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 na kukamilika kwake kwa kiasi kikubwa kutapunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Mwanza.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za dhati za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Serikali inatekeleza miradi hii ili kuhakikisha huduma za msingi za kijamii zinapatikana kwa wananchi wote,” amesema.

Mhe. Dkt. Mpango ameyataja maeneo yakayaonufaika na mradi huo kuwa ni pamoja na Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwanhima, Fumagila, Sahwa, Igoma, Kishiri na Nyamhongolo. Aidha amesema maeneo ya Usagara, Nyashishi na Fella katika Wilaya ya Misungwi pamoja na maeneo ya Kisesa, Bujora na Isangijo katika Wilaya ya Magu pia yatanufaika.

Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akizungumza katika hafla hiyo amesema Lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, huduma ya maji kwa maeneo ya Mijini inafika asilimia 95 na maeneo ya vijijini asilimia 85.

Amesema Wizara inatambua kuwa Jiji la Mwanza linakuwa kwa kasi na kwamba pamoja na mradi huo kuzalisha lita za ujazo milioni 48 kwa siku, Serikali kwa kushirikiana na wadau wake wa kimaendeleo itaendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo pamoja na uboreshaji wa chanzo cha Maji cha Capripoint ili kiweze kutosheleza mahitaji kwa Jiji la Mwanza ambalo kwa sasa linahitaji lita milioni 160 kwa siku.

"Natambua kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi Mwanza (MWAUWASA), wanapambana usiku na mchana katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa nzuri," Mhe. Aweso amesema wakati akizungumzia hali ya huduma ya majisafi jijini Mwanza.

Mhe. Aweso (Mb) amebainisha kuwa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya majisafi nchini yenye lengo la kuhakikisha huduma ya Majisafi, salama na yenye kutosheleza inawafikia wananchi wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news