TIBA SARATANI IPO

NA LWAGA MWAMBANDE

SEPTEMBA 13, 2022 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango alizindua jengo la wagonjwa wa saratani la Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Bugando jijini Mwanza.

Aidha,Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt.Fabian Massaga alisema ujenzi wa jengo hilo lenye uwezo wa kulaza wagonjwa 120 kwa siku ulianza Agosti, 2020 kwa gharama ya shilingi bilioni 5.6.

Jengo hilo linatarajiwa kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa ambao walikuwa wanasafiri kwenda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, wakiwemo wale waliokuwa wanakodi vyumba wakati wakisubiria matibabu ya saratani Bugando. Ungana na mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande upate maarifa kupitia shairi hapa chini kuhusu uwekezaji huu;

1:Asante kwa Serikali, ugonjwa wa saratani,
Kutupatia mahali, tiba karibu nyumbani,
Tusiende mbali sana, huku tukiwa shakani.
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

2:Mkono wa Serikali, umeingia kazini,
Vile unajali hali, Kanda hii ya Ziwani,
Wewe nenda sipitali, huduma hospitalini,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

3:Kusafiri hadi mbali, Dar es Salaam jijini,
Kusaka hospitali, kwa wagonjwa saratani,
Mbali sana tena ghali, kwa sasa ni ahueni,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

4:Makamu Rais kweli, Mpango Mwanza jijini,
Amekwenda sipitali, kwa jengo la saratani,
Amekitoa kibali, watu waende kazini,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

5:Ugonjwa huu mkali, uitwao saratani,
Kuugundua ni ghali, ukiingia mwilini,
Hata tiba yake ghali, ni shida sana mwilini,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

6:Tunaambiwa ukweli, tusiingie shidani,
Ukiziona dalili, zanyemelea mwilini,
Mapema pata akili, kapime sipitalini,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

7:Kuwahi hospitali, kugundua saratani,
Kupona kwetu kivuli, gonjwa hili saratani,
Kuchelewa shida kweli, kwa tiba ya saratani,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

8:Kuepuka janga hili, Mikoa Kanda Ziwani,
Twende kamili kamili, kupima sipitalini,
Wakigundua dalili, tiba huwa ahueni,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

9:Ocean Road fadhali, itapata ahueni,
Waendao sipitali, ni rufaa za mwishoni,
Hata safari si mbali, Bugando iko jikoni,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

10:Imetoa Serikali, mia tano milioni,
Kanda ya Ziwa si hali, magonjwa ya saratani,
Jengo la hospitali, kwa sasa liko kazini,
Hospitali Bugando, tiba saratani ipo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news