Serikali yatoa maagizo kuhusu majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi

NA ROTARY HAULE

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amezindua mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi nchini.
Dkt.Gwajima amezindua mwongozo huo Septemba 11,2022 katika Kongamano maalum lililofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo kwa Mfipa Kibaha mkoani Pwani.

Dkt.Gwajima amezindua mwongozo huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye alipaswa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mwongozo huo.
Akizungumza wakati akizindua mwongozo huo Dkt.Gwajima amesema kuwa , mwongozo huo utasaidia kufungua fursa za wanawake katika kuendeleza biashara zao na hivyo kukuza uchumi katika familia zao.

Amesema kuwa,majukwaa hayo yalikuwepo lakini yalikuwa hayafanyi kazi kwa ufanisi lakini mwongozo huo utasaidia majukwaa hayo kufanya kazi kwa ufanisi kuanzia Taifa, mikoa,wilaya,kata,vijiji na hata vitongoji.

"Majukwaa haya yaende vijijini kusaidia wanawake wanaoshinda mashambani ili waweze kutambua fursa za kiuchumi zilizopo nchini ili nao waweze kuwa na uchumi imara kupitia shughuli zao za kijasiriamali,"amesema Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema Serikali itafuatilia kila halmashauri ili kujua kama mwongozo huo unatumika ipasavyo sambamba na kuhakikisha majukwaa hayo yanaundwa mpaka vijijini.

Amesema kuwa,Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuwaimarisha wanawake kiuchumi na kwamba tangu aingie madarakani mambo mengi na makubwa yamefanyika.

"Mpango huu ulianzishwa na Mheshimiwa Rais wakati akiwa Makamu wa Rais na mara baada ya kuchukua kiti cha Urais aliandaa programu ya Kitaifa ya kuleta usawa kiuchumi ndio maana majukwaa ya Wanawake yamekuwa imara zaidi, kwahiyo lazima tumpongeze Rais wetu,"amesema Dkt.Gwajima.
Amesema,katika kuimarisha majukwaa hayo Serikali imekuwa makini na yapo mambo yamefanyika ikiwa ni pamoja na kufanyia marekebisho Sheria za Fedha katika mamlaka za Serikali ya Mitaa.

Amesema, mengine ni kutoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali kwa Wanawake ,kuwezesha Wanawake kupata masoko ya kuuzia bidhaa zao pamoja na kuendelea kutoa mikopo ya kuendeleza bidhaa zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, Pwani imejipanga vizuri katika kuyaimarisha majukwaa hayo na kwamba mpaka sasa tayari zaidi ya shilingi bilioni 5 zimetolewa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Kunenge, amesema mpaka sasa Mkoa wa Pwani tayari umeunda majukwaa 1,722 ambapo kati ya hayo majukwaa 980 yamesajiliwa na kwamba kupitia mwongozo huo Pwani itafanya vizuri zaidi.
Hata hivyo,Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Zainabu Chaula,amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kwani yatakwenda kuleta usawa hasa katika uchumi .
Chaula amesema kuwa, wizara itahakikisha inaleta tija kwa wanawake kama ambavyo malengo ya Rais yalivyokusudiwa huku akiwaomba Wanawake kote nchini kuhakikisha wanajiunga katika majukwaa hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news