TASAF yagusa maisha ya wananchi Nyamatare

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Kata ya Nyamatare Manispaa ya Musoma mkoani Mara wanaonufaika na Mpango wa TASAF wamesema, wameendelea kupata manufaa mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto wao, kufanya shughili za ujasiriamali, ufugaji kutokana na fedha wanayopewa hatua ambayo inazidi kuchochea uchumi wao kuendelea kuimarika na kubadilisha hali zao kimaisha.
Wamesema, TASAF imekuwa mkombozi wa maisha yao ambapo kabla ya kuanza kunufaika na mpango huo, maisha yao yalikuwa magumu hasa kiuchumi, lakini kwa sasa wana mabadiliko makubwa na wanaishukuru Serikali kuleta mapango huo ambao umeendelea kuwaneemesha na kuwafanya wathaminike katika jamii.

Wameyasema hayo Septemba 15, 2022 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI BLOG wakiwa katika Ofisi ya Kata ya Nyamatare ambapo Maafisa kutoka TASAF Manispaa ya Musoma waliweza pia kutoa elimu kwa walengwa, kufanya zoezi la uhuishaji fedha kwa walengwa ambao hawajapokea fedha na kusainisha walengwa waliopokea fedha kupitia mitandao na benki.

Belitha Malulu ( 76) ambaye ni mnufaika wa mpango huo amesema kuwa, kwa sasa ana mudu kuwanunulia mahitaji ya shule wajukuu zake wawili ikiwemo unifomu, daftari, kalamu na kuwagharamia matibabu pindi wanapougua na kwamba wanaendelea vyema na masomo yao ya elimu ya msingi na kwamba, TASAF imempa nguvu na uhakika wa maisha.
"Wajukuu wangu hawakosi kalamu, daftari, wala unifomu hawakosi vipindi darsani, hali yangu kiuchumi ilikuwa mbaya sana kabla ya kuingia kwenye mpango, kwani binti yangu aliondoka nyumbani zamani na kuniachia na watoto wake wawili (wajukuu) akawa anatuma pesa kidogo, lakini ikafikia wakati akaacha kabisa kutuma akawa hapatikani hewani. nilipoingia kwenye mpango nimehakikisha fedha hii inafanya kile ambacho kinatakiwa wajukuu wasome, wapate mahitaji ya shule na kiasi kingine ninawanunulia chakula zamani hata unifomu ilikuwa shida kuwanunulia,"amesema Malulu.

Moshi James Ogunya amesema kuwa,fedha anayoipata imemfanya ajishughulishe na biashara ya kuuza dagaa ili amudu kuendesha maisha yake ikiwemo kuwahudumia watoto wake watatu kwani mume wake aliachana naye miaka sita iliyopita kabla ya kuanza kunufaika na mpango huo alikuwa akiishi maisha magumu, kwani hakuwa na mtaji wowote wa kumuwezesha kufanya biashara alijikita kufanya vibarua wakati vinapokosekana hakuwa na mbadala.

"Niliishi maisha magumu sana, lakini baada ya kuingia kwenye mpango, nimejikita kufanya biashara ya dagaa. Kila siku ninaamka asubuhi nakwenda ziwani (Victoria) nanunua naanika baadaye napeleka kuuza gengeni, kwa sasa uhakika wa kupata chakula cha wanangu upo mkubwa, matibabu, wanasoma vizuri kabisa.

"Mungu akijalia nataka kuanza kufuga kuku ili nikija kuondoka kwenye mpango niwe na hali nzuri kimaisha uhakika wa faida shilingi 8,000 hadi 11,000 kwa siku ninao na TASAF ndio nimepatia mtaji huo na hii ni baraka na neema kwangu,"amesema Moshi James.
Magreth Peter ameishukuru Serikali kuanzisha TASAF ambapo amesema, imekuwa na manufaa kwa wananchi ambao hawakuwa na uwezo wa kusomesha watoto wao wala mitaji ya kuwawezesha wafanye shughuli za ujasirimali kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.

"Mimi kwa sasa nafanya ujasiriamali nauza mboga mboga, nina watoto wanne, mume wangu alifariki nikawa naishi kwa tabu ndugu zangu hawakunisaidia chochote zaidi ya kuniachia mzigo wa kulea watoto wangu.

"Lakini TASAF naishukuru baada ya kuwa nimeingizwa kwenye mpango nilipoanza kupewa fedha nikaanza kuuza mboga mboga kwa sasa maisha yangu yamekuwa na ahueni kubwa watoto wanasoma na kupata mahitaji yote namidu kulipa kodi ya nyumba,"amesema Magreth.
Ibrahimu John ni Mwezeshaji Kutoka TASAF Manispaa ya Musoma amewataka walengwa wa mpango huo kuendelea kuzitumia fedha wanazozipata kama mbegu ya kujiletea manufaa na maendeleo ili wainuke kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali zenye tija.

"Niwahimize walengwa waendelee kuzitumia hizi fedha kwa manufaa, anayefanya ufugaji afuge apate mayai ambayo akiyauza yatabadilisha maisha yake, kwenye kilimo pia watumie fedha hizi kuzalisha, na hata upande wa ujasiriamali wazitumie kufanya shughuli hizo kikamilifu kusudi maisha yao yabadilike kama ambavyo Serikali imedhamiria, watoke chini waje kuwa na uchumi bora na hili linawezekana iwapo malengo watayazingatia kikamilifu nasi tunawapa elimu wazidi kufikia malengo," amesema Ibrahimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news