TUUCHAGUE MFUMO-2:Zote zinapata kitu, kutoka wadhamini wetu

NA LWAGA MWAMBANDE

SOKA la Tanzania linalipa, huo ndiyo ukweli. Na kwa kuthibitisha hilo turejee uamuzi wa Kampuni ya Azam Media Limited kuingia mkataba wa haki za matangazo ya televisheni katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mkataba huo wa hivi karibuni wa miaka 10 wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 200, kama alivyosema Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Muhando ulitokana na uzoefu wao wa miaka minane katika kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ambako walijifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuona jinsi timu zinavyojiendesha na changamoto zake.

Kampuni ya wazawa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika soka la ndani ni ishara njema kuwa, soka letu lina ubora wa kipekee ambao kila mmoja akiutumia kwa ufanisi iwe timu au klabu unaweza kutoa matokeo bora kwa pande zote.

Ndiyo maana, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anarejea wito wake kuwa, yafaa sasa tuchague mfumo ambao utatutambulisha sisi kwa ubora wetu na ushindani ambao utaongeza ufanisi na matokeo ya haraka kuanzia ngazi za chini hadi juu, jifunze kupitia shairi hapa chini;


1.Kuna kitu hapa kwetu, mambo yanakuwa kwatu,
Japo tofauti kwetu, badobado ni kubwa tu,
Azam Tivii yetu, yake kwetu mambo kwatu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

2.Angalau sasa kwetu, zapendeza timu zetu,
Zote zinapata kitu, kutoka wadhamini wetu,
Ona usajili wetu, kwa kiasi bora kwetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

3.Mwaka huu hapa kwetu, wengi wadhamini wetu,
Timu usajili kwatu, bora ushindani wetu,
Tishio kwa timu zetu, kushinda makombe yetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

4.Kwa mfano huku kwetu, timu nne juu kwetu,
Simba Yanga hizo zetu, miaka mabingwa wetu,
Hata sasa ni bora tu, kuzidi zingine zetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

5.Azam ni timu yetu, ndiyo matajiri wetu,
Yatimiza ligi yetu, tena mdhamini wetu,
Singida Big Stars tu, mwaka huu ina vitu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

6.Ni Geita Gold tu, hizo timu tano zetu,
Kiuchumi ziko kwatu, tofauti zile zetu,
Yapendeza ligi yetu, huu ushindani wetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

7.Marekani iwe yetu, yale yao yaje kwetu,
Ziwe sawa timu zetu, kwa tofauti chache tu,
Tuchangamke kivyetu, michezo uchumi wetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

8.Uingereza si kwetu, kulivyo uduni wetu,
Kwanini timu chache tu, ziwe zinashinda vitu,
Huku nyingi roho kwatu, kuwa ni washiriki tu?
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

9.Kwa maendeleo yetu, sibaki timu mbili tu,
Yanga Simba hizo zetu, na hata nyingine ni zetu,
Zidiwepo kati yetu, zinazosindikiza tu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

10.Kufikia lengo letu, tusijifungie katu,
Marekani nako kwetu, Hispania ni kwetu,
Kote huko kuna vitu, bora kwa mpira wetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news