UGANDA NA TANZANIA, LIJENGENI BOMBA LENU: Zile ni Siasa tu, Hata Bunge ni maoni, yamekuja tumefuta

NA LWAGA MWAMBANDE

BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Manfredo Fanti ameeleza msimamo wa umoja huo katika ujenzi unaoendelea wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kufuatia azimio la Septemba 14 la Bunge la Umoja wa Ulaya kulaani utekelezaji wa mradi huo kwa madai ya wasiwasi wa uharibifu mazingira na athari mbaya kwa maisha ya binadamu.

Hayo ameyabainisha kupitia mahojiano maalum aliyofanya na Gazeti la Mwananchi ambapo wakati akijibu moja wapo ya swali alisema, huo ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa wa Bunge la Ulaya, ambao ni halali kabisa ndani ya bunge la Ulaya, lakini hawalazimishi.Soma kwa kina hapa

Balozi Fati amesema,mamlaka nchini Tanzania na Uganda ziko huru kuendelea na mradi kwa sababu hayo ni mataifa huru na yana haki ya kuamua kuhusu sera zao za nishati na maendeleo. Ungana na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande upate maarifa kidogo hapa chini;

1:Balozi kasema vema, hili Bomba la Mafuta,
Linalofanywa ni jema, nchi zizidi takata,
Bunge Ulaya kusema, mradi halijafuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

2:Ni balozi wa Ulaya, gazeti limtafuta,
Akasema bila haya, maneno yaliyopita,
Kwamba Bunge la Ulaya, ni siasa si utata,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

3:Bunge tulilisikia, tamko lilivyopita,
Mradi likisagia, ya kwamba una utata,
Mazingira watishia, nchi bora zikafuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

4:Hatukuwanyamazia, kwa huo wao utata,
Uganda na Tanzania, matamko yalipita,
Ya kwamba zimepania, hilo bomba la mafuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

5:Hoima linaanzia, hilo Bomba la Mafuta,
Uganda nakutajia, kwingi kwingi litapita,
Kupitia Tanzania, Bandari Tanga ukuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

6:Balozi Fanti kusema, hili bomba la mafuta,
Kweli amesema vema, kwa hayo yaliyopita,
Ambayo tumeyasoma, na tayari tumefuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

7:Bomba la mafuta ghafi, nchi mbili litapita,
Mazingira ni masafi, shida hazitatupata,
Kote huko mtu hafi, bomba litakakopita,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

8:Uganda na Tanzania, si kukurupuka hata,
Athari wamepitia, tuwezazo kuzipata,
Hali wameiridhia, kwamba hakuna matata,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

9:Watu kutoa maoni, hatujaweka ukuta,
Hata Bunge ni maoni, yamekuja tumefuta,
Wajue tuko mbioni, kujenga bomba mafuta,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

10:Uchumi twaangalia, ambao tutaupata,
Mradi ukiingia, kujenga bomba mafuta,
Kote litakopitia, fursa watazipata,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

11:Uganda imeshasema, laja bomba la mafuta,
Tanzania imesema, twajenga bomba mafuta,
Na balozi amesema, Bunge haliwezi futa,
Uganda na Tanzania, lijengeni bomba lenu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

1 Comments