VIFAFIO yazindua mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara limezindua mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane kuanzia Septemba 2022, hadi Aprili 2023 katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na utagharimu jumla ya shilingi milioni 37 kwa halmashauri zote.

Mradi huo unatekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society ukilenga kufikisha elimu ya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mialo ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ambapo katika halmashauri ya Wilaya ya Musoma utatekelezwa katika kata saba ikiwemo Bukima, Bukumi, Rusoli, Nyamrandirira, Bwasi, Msanja na Kiriba na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda utatekelezwa katika kata tatu.
Hayo yamebainishwa Septemba leo 22, 2022 na Meneja wa Shirika hilo, Majura Maingu wakati wa uzinduzi wa mradi huo kwa viongozi mbalimbali wakiwemo watendaji wa kata, viongozi wa Halmashauri ya Musoma na ngazi ya Mkoa katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Amesema kuwa, mradi huo waliomba kwa mfadhili utekelezwe kwa miaka mitatu kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 walizoomba lakini wamepewa shilingi milioni 37 watekeleze kwa kipindi cha miezi nane. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa maeneo husika ambayo mradi huo unatekelezwa ili uwe na tija kwa jamii.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Robinson Wangaso amesema kuwa, mradi huo utahusisha kutoa elimu kwa wavuvi maeneo ya mialo, kutumia michezo kutoa elimu, kufanya mikutano ya hadhara na wavuvi, kufanya majadiliano na wadau pamoja na kuunda klabu za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Amesema, mradi huo unatarajia kuleta matokeo ikiwemo kuwafanya wanawake na watoto wachukue hatua kwa kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwa mamlaka za serikali na jamii iwe na uwezo wa kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kuimarisha mfumo bora katika kamati za vijiji na kata zinazohusika na kupinga vitendo hivyo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba amelitaka shirika hilo kutekeleza mradi huo hasa kwa kujikita zaidi kutoa elimu ya usawa wa kijinsia ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa wanawake na watoto kuwapa elimu ya kuripoti matukio ya ukatili wanapofanyiwa bila kikaa kimya.

Amesema, mwanamke amekuwa akichukuliwa kama chombo cha starehe na wakati mwingine hathaminiwi katika jamii, hivyo amesisitiza mradi huo uwaelimishe zaidi wanawake kupaza sauti zao kutoa taarifa katika mamlaka za serikali ikiwemo Ofisi za Ustawi wa Jamii, maendeleo ya jamii Ofisi za Vijiji, kata, Polisi juu ya matukio wanayofanyiwa ya ukatili wa Kijinsia bila kuvifumbia macho.
Ameongeza kuwa, Mkoa wa Mara vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vipo vikihusisha ukatili wa kingono, kisaikolojia, kimwili, ukatili wa kiuchumi pamoja na vitendo vya ulawiti na ubakaji. Hivyo juhudi lazima ziendelee kufanywa na wadau wote kuhakikisha vitendo hivyo vinamalizika.

"Elimu iendelee kutolewa kuanzia chini kabisa ngazi ya familia Baba na Mama watoe usawa wa majukumu kuanzia kwa watoto wao kufanya kazi mbalimbali. Hii itasaidia wakiwa watu wazima watajua kuishi katika usawa kwani watakuwa wanafahamu kutokana na msingi waliojengewa,"amesema.
Amesema, maendeleo katika jamii hayawezi kufanikiwa kwa ufanisi pasipo kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia na pia amesisitiza miradi ya ukatili inapotekelezwa iwe na mikakati ya kuwa endelevu na ilete matokeo chanya kwa walengwa.

"Katika mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto una maeneo nane, kwanza ni kuimarisha uchumi wa kaya uchumi wa kaya ukiwa thabiti ukatili utaisha, pili mila na desturi hapa mila ambazo hazifai ziachwe na nzuri ziendelezwe na tatu ni mazingira salama hapa lazima mazingira yawe salama kwa wote bila mwingine kufanyiwa ukatili kwani mwanake hata ukimpa shilingi milioni 10 kama amekatwa mkono haitasaidia cha msingi ni kumaliza vitendo vya ukatili kwa maendeleo,"amesema Neema Ibamba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma amesema ujio wa mradi huo katika halmashuri hiyo utasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mialo, visiwa na kusaidia kuimarisha usawa wa kijinsia na uwajibikaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news