Wananchi wa Pwaga Jimbo la Kibakwe kusahau shida ya maji

NA MWANDISHI WETU

WANANCHI wa Kata ya Pwaga wanatarajia kuanza kunufaika na mradi mpya wa maji baada ya Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa maji kupitia Mkandarasi Pioneer Building Limited.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akishuhudia uwekaji wa saini kati ya Mkandarasi Pionner Buiding Limited, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mpwapwa,Mhandisi Cyprian Warioba, na Mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Mkoa Bi.Priscilla Mkilanya.

Hayo yamefanyika wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene alipokabidhi nakala ya Mkataba wa Ujenzi wa mradi huo maji unaotarajia kukamilika baada ya siku 365, kwa Diwani wa Kata ya Pwaga, Mhe.Wilfred Mgonela katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Pwaga jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Mpwapwa.

“Nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha nyingi kiasi cha Billioni 4.3 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ya maji katika kata ya Pwaga utakaosaidia vijijji vitano vya, Maswala, Itende, Ng’onje, Mungui na Pwaga,”alisema Waziri.

Lazima tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi wa maji na kwa uwazi ili wote tuwe na uwezo wa kuona kilichopo na kuondoa mianya ya vitendo vya udanganyifu katika utekelezaji wake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akimkabidhi Diwani wa Pwaga Mhe Wilfred Mgonela nakala ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Maji mara baada ya kusainiwa na mkandarasi Pionner Buildings Limited.

“Mradi huu utatoa ajira nyingi kwa wananchi ambazo zitasaidia kujenga uchumi wa kata ya Pwaga,"alisema.

Aidha, Waziri ametoa wito kwa Mkandarasi Pioneer Building Limited kutekeleza mradi wa maji kwa kasi ili watu waanze kupata huduma ya maji.

Amehimiza mfumo wa uongozi, wa maji kata ya Pwaga kusukwa upya ili uweze kusimamia vizuri mradi wa maji na uendane na sera pamoja na sheria ya maji.

Naye Diwani wa Kata ya Pwaga, Mhe.Wilfred Mgonela ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha za Utekelezaji wa mradi wa maji.
Mhe. Wilfred Mgonela akimkabidhi Mtendaji wa Kata ya Pwaga, Bi. Moteswa Mnyambwa nakala ya Mkataba ya Utekelezaji wa Mradi wa Maji mara baada ya kusainiwa na mkandarasi Pionner Buildings.

“Naomba watendaji na wananchi tushirikiane kusimamia vyema mradi ili yasije yakajitokeza mapungufu katika utekelezaji wa mradi,”alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mwl, Jakson John amesema kukamilika kwa mradi wa maji Pwaga utasaidia afya za watu kuimarika.

“Sisi tunaosimamia sekta ya elimu kwa upande wa shule ya Msingi tunawanafunzi 5000 ambao watakaonufaika na mradi huu wa maji”

Katika taarifa yake Meneja wa RUWASA Halmashauri ya Mpwapwa, Mhandisi Cyprian Warioba amesema shughuli zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Rufu, ujenzi wa tenki moja lenye uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 za maji litakalojengwa kijiji cha Ng’onje, kutakuwa na ujenzi wa tenki la pili la maji wa lita 50,000 litakalo jengwa kijiji cha Itende.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika picha alipotembelea eneo linalotarajia kujengwa tenki la maji lenye uwezo kubeba lita 500,000 katika kijiji cha Ng’onje kilichopo jimbo la Kibwake Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

“Kutakuwa na ujenzi wa Ofisi moja kwa ajili ya uendeshaji na uendelevu wa mradi itakayotumiwa na viongozi watakaosimamia zoezi zima la uendeshaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na vituo vya kuchotea maji 27 pamoja na Marambo manne ya kunyweshea mifugo.

"Tunakusudia kukamilisha mtandao wa bomba jumla ya km 61, ambazo km 15 ni kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki la Ng’onje na km 43 ni mtandao kwa maeneo yote kwa maana ya vijiji vyote vinavyohusiana na mradi Itende, Pwaga, Mungui pamoja na Maswala,"alisema Mhandisi huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news