Balile awauma sikio wanahabari

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatius Balile amewaasa waandishi wa habari nchini kuendelea kusimama imara katika kutetea taaluma na maslahi yao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na ubora.

"Vyombo vya habari vinafanya kazi ya kujenga uelewa katika jamii, kuwezesha wananchi kufanya maamuzi kutokana na uelewa walionao kwa ajili ya maendeleo,pia vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana ya kubadilisha mitazamo na maisha ya watu kwa haki ya kupata habari ambayo hupelekea haki nyingine kupatikana;

Balile ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TEF yakiangazia uchechemuzi wa sheria za habari nchini.

Amesema, waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele kuandika na kuripoti kuhusu masuala ya wengine, lakini kwa upande wao mambo yamekuwa hayaridhishi, hivyo wana jukumu kubwa la kutetea taaluma yao na maslahi yao kwa ujumla.

Pia amesema, licha ya shauku ya wengi kutaka kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zipo baadhi ya sheria ambazo zinasababisha washindwe kufanya kazi zao kwa weledi na hivyo kushidwa kutetea haki na maslahi yao nchini.

Amesema, waandishi wa habari wenyewe ndio wamavaa viatu na wanafahamu mazuri na mabaya wanayokutana nayo kwenye tasnia, hivyo wakiandika na kuyasemea matatizo wanayokutana nayo itaifanya Dunia itambue changamoto za waandishi wa habari.

"Kuna baadhi ya taasisi zinasema wanatetea haki za waandishi, lakini wao sio waandishi na hawazijui changamoto za waandishi ndio maana tukasema tuanze kutetea haki na maslahi yetu wenyewe kwa ustawi bora wa tasnia hii.

"Ili kutetea haki zetu zipatikane tukiwa na hali nzuri basi tutakua na nguvu ya kutetea haki za wengine kwa ufasaha pia tuondoe ile kasumba ya kwamba wanahabari hatuandiki habari zinazotuhusu,"amesema.

Wakati huo huo,Balile amesema, wadau wa habari nchini wakiwemo TEF wapo katika mchakato wa kuwaomba watunga sheria ili vifungu ambavyo vinaonekana kuwa kikwazo kwa wanahabari na tasnia kwa ujumla viweze kuondolewa au kufanyiwa maboresho ili kuifanya taaluma hiyo kuwa imara nchini.
Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mheshimiwa Wiebe de Boer amesema,uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa maendeleo kiuchumi na ustawi bora wa demokrasia.

"Uhuru wa habari ni nguzo muhimu katika ustawi wa demokrasia na kuchochea maendeleo ya taifa.Demokrasia kamilifu inategemea upatikanaji wa taarifa kwa uwazi na za kuaminika.

"Vivyo hivyo, ustawi wa maendeleo unategemea taarifa sahihi na za kuaminika, hivyo nichukue nafasi hii kuipongeza TEF kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya umuhimu wa maboresho ya sheria za habari nchini.

"Na tumeona juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali, Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) ameonesha dhamira njema katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, nasi tutaendelea kuunga mkono juhudi hizo,"amesema.

Wakati huo huo, mwenyekiti mstaafu wa TEF, Theophil Makunga amesema, waandishi wa habari ni watu muhimu katika kushiriki kuwezesha upatikanaji wa maendeleo endelevu katika jamii na Taifa kwa ujumla.

"Ninaamini kwamba tunapoelekea kuna mwanga unaonekana mbele wa kuwafanya waandishi wa habari waweze kufanya kazi kwa uhuru ili kuleta maendeleo ya nchi.Unapompa uhuru mwandishi wa habari unamsaidia kuchuja mambo ya kuandika na ambayo hayafai kuandikwa kwa uhuru wake, lakini ukiweka sheria ambazo zinazomzuia hawezi akafanya kazi vizuri,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news