Balile:Wadau wa habari tunatarajia Bunge la Novemba lifanye jambo

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile amesema, wadau wa habari nchini wana matumaini makubwa kwamba muswada wa maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 utawasilishwa bungeni Novemba,mwaka huu.
Balile ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na TEF kwa wanahabari na washauri wao ili kubadilishana mawazo na kujadiliana namna ya kuboresha habari zinazohusiana na kampeni ya utetezi wa Sheria ya Huduma za Habari nchini.

"Hatutaki kuamini kwamba muswada utapelekwa bungeni Februari mwakani, bali tunaamini kuwa muswada huo utapelekwa bungeni katika Bunge la Novemba, mwaka huu. Kwani, Agosti 11 na 12, mwaka huu tulikutana na Serikali, tulijadiliana na kuelezana kuna vifungu vinahitaji marekebisho,"amesema Bw.Balile.

Mwenyekiti huyo ameyasema hayo ikiwa ni miezi kadhaa imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo kuhusu sheria za habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru wa vyombo vya habari nchini kufanyiwa maboresho.

Rais amesema

Rais Samia alitoa maelekezo hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

Tunasubiria

Wakati huo huo, Bw.Balile amesema, miongoni mwa vifungu hivyo ni pamoja na kile cha 1 hadi 37 ambapo pia wadau wa habari nchini wanasubiria kukutana na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Nnauye katika kikao cha mwisho.

"Mheshimiwa Waziri Nape alipenda kikao cha mwisho na yeye ashiriki kujadiliana na wanahabari na wadau waliopo kwenye taaluma hii, ili kuona ni kipi kiwepo kwenye sheria, hivyo tunasubiri kikao hicho. Bunge la Septemba, mwaka huu muswada haukufanikiwa kwenda bungeni, lakini tunaamini baada ya kikao hicho muswada utawasilishwa Bunge la Novemba, mwaka huu,"amefafanua.

Waziri Nape

Agosti 26, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliwahakikishia wadau wa habari kuwa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari nchini hayatapelekwa bungeni bila pande zote kukubaliana na kuridhika.

Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye katika mjadala wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC ambao uliangazia kuhusu mapendekezo hayo.

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Lengo kuu

Katika hatua nyingine, Bw.Balile amesema kuwa, lengo la mchakato huo ni kuwezesha marekebisho kadhaa ya vifungu vya sheria hiyo ili kuwezesha taaluma hiyo kutekeleza majukumu yake bila kukumbana na vikwazo.
"Si wanahabari tu wanafurahia uhuru wa kujieleza na kupokea habari, wenzetu Kenya kuna uhuru ni nchi jirani, unaona wameweza, sisi tuna kosa gani tusifikie huko, lakini haki inakuja na wajibu, inawezekana kukapata marekebisho au maboresho hayo ila kuna msemo siku hizi wanasema isiwe kama fungulia mbwa, bado wanataaluma wanapaswa kwa mujibu wa sheria kufanya kazi hiyo kwa weledi na misingi ya kitaaluma.

"Hatua hiyo itawatofautisha na wale wengine wanaoamka asubuhi na kuanzisha blogu, kundi au njia yoyote ya kutoa habari kwenye mtandao na kuanza kuiburuza nchi,wananchi pia bila kufuata maadili na misingi ya taaluma.

"Sisi (Watanzania) tuna tamaduni zetu, maadili yetu na kanuni ambazo zinatuongoza, tunatarajia wanahabari watafanya kazi ambayo iutawatofautisha na wale wa kwenye mitandao, kwani kw asasa baadhi ya watu wanashindwa kutofautisha wale wa mitandao na wanahabari, unakuta anaongoza nchi kwa kuleta habari, lakini hazijafuata ile misingi inayopaswa kutuatwa kitaaluma,"amesema Balile.

Rai ya Bw.Balile inaendana sambamba na wito wa Rais Samia ambaye pia Mei 3,2022 alishauri waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa kuandika mambo mazuri ya kutetea Bara la Afrika huku akiwataka waandishi wa habari kuzitangaza mila na desturi nzuri za Tanzania.

“Tunazo mila na desturi tunapaswa kuzilinda, na nyinyi waandishi wa habari mnatakiwa kuzilinda ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Baadhi ya watu wanaposti picha chafu mtandaoni, wanajianika mtandaoni, wengine wanafanya hivyo kwa kutojua madhara ya kufanya hivyo,"alisema Rais Samia.

Hata hivyo, Mheshimiwa Nape katika mahojiano hayo na BBC alifafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.

"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na nimeridhika,sasa tutakwenda kikao cha pili ambacho nitalazimika kwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"alisema Mheshimiwa Nape.

Meena

Kwa upande wake Bw.Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF katika semina hiyo aliwaeleza waandishi wa habari umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya karibu na washauri wao ili kuinua ubora wa taarifa wanazozichapa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Bw.Meena amesema, mshauri anajitolea sehemu ya wakati wake ili kumsaidia mwanahabari na kumjenga kwa manufaa ya sasa na hata hapo baadaye.

"Hivyo, ni vizuri kuwa na mawasiliano ya karibu na mshauri wako, tunapaswa kuwa na stori ambazo hata hapo baadaye, wengine watakaokuja watajua kuna kazi iliyofanywa. Kwa kiwango kikubwa katika ushirikiano huu, mwanahabari anaweza kufaidika kwa kiwango kikubwa endapo atafanya kazi kwa karibu na mshauri wake,’’amesema Bw.Meena huku akiungwa mkono na washiriki wote ukumbini hapo.

Wakili

Naye Wakili msomi wa kujitegemea, James Marenga amesema,sheria rafiki kwa vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo muhimu ambayo itawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma nchini.

Wakili Marenga aliyasema hayo hivi karibuni katika semina ya siku moja iliyoratibiwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa waandishi wa habari za mtandaoni iliyofanyika katika Hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam.

Kupitia semina hiyo, Wakili huyo aliwapitisha wanahabari katika vifungu mbalimbali vya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 vikiwemo vile ambavyo vinaonekana kuwa chanya kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.

Sambamba na vifungu ambavyo wadau wanaona kuna haja ya Serikali kuvifanyia maboresho au kuvifuta kabisa kwa kuwa, vina changamoto ili kuiwezesha tasnia ya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news