WAZIRI MKENDA AKERWA KUSUASUA UJENZI VETA-SIMIYU,ATOA MAAGIZO MRADI UKAMILIKE HARAKA

NA MATHIAS CANAL-WEST

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof. Adolf Mkenda (Mb) amekerwa na kusuasua kwa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi-VETA mkoani Simiyu.
Ameagiza wataalamu wote wa usimamizi wa chuo hicho ambao ni kutoka Chuo cha ufundi Arusha waweke kambi mkoani Simiyu ili kukagua na kukamilisha haraka ujenzi huo.

Waziri Mkenda ametoa maagizo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, Oktoba 8, 2022.
"Tungependa kuona chuo cha ufundi Arusha kikisimamia kazi hadi watu binafsi wawatafute kwa ajili ya kwenda kusimamia ujenzi, lakini hapa sidhani kama wamefikia kiwango kizuri, wamejitahidi lakini hawajafikia kwa hiyo siridhiki,”amesema Waziri Mkenda.

Chuo cha Ufundi stadi VETA-Simiyu ni miongoni wa vyuo vinne ambavyo vimesalia kukamilika ujenzi wake ili mikoa yote iwe na vyuo vya Ufundi VETA, Waziri Mkenda ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Simiyu, Rukwa, Njombe, na mkoa wa Songwe ambao fedha tayari zimepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Prof .Mkenda amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora katika ujenzi wa Vyuo hivyo na kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa na serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.

Pia, Waziri Mkenda amesema kuwa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafiri, serikali itaendelea kuzitatua.
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa kwa sasa Wizara imejipanga kuanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya zote nchini hivyo kama ujenzi wa usimamizi wa vyuo vya mikoa unasuasua ni wazi kuwa kusimamia Wilaya zote nchini haitakuwa kazi rahisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news