Bilionea Rostam Aziz afunguka kuhusu Hayati Maalim Seif

NA DIRAMAKINI

MFANYABIASHARA Bilionea wa Kitanzania na Mbunge wa zamani, Rostam Aziz amesema, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa uhai wake alikuwa miongoni mwa viongozi wenye haiba za kipekee ambao wataendelea kuenziwa kizazi baada ya kizazi.

Rostam ameyasema hayo Oktoba 22, 2022 katika Hoteli ya Golden Tulip katika Mkutano wa Pili wa Kuenzi Urithi wa Maalim Seif Sharif Hamad.

"Ulipokuwa unakaa na Maalim Seif Sharif Hamad ulikuwa unahisi hasa kuwa umekaa na Kiongozi. Hakuhitaji hata kusema chochote. Uwepo wake popote alipokuwepo ulidhihirisha uwepo wa Kiongozi, tena Kiongozi kwa maana hasa ya Kiongozi. Haiba, bashasha, utulivu, maarifa, weledi, na muhimu kuliko yote, hekima na busara,vyote hivi ulikuwa ukivihisi na kuviona kila alipokuwepo.

"Hayo si ya kuhadithiwa na wengine, nimeyahisi na kuyaishi mimi mwenyewe nilipokuwa nikikutana na Maalim Seif.

Pengine wengi mnaweza kustaajabu kuwa ni kweli Rostam alipata kukaa pamoja na Maalim Seif kiasi hicho hadi kuweza kumjua na kumzungumza hivi ninavyomzungumza hapa leo? Jibu lake ni NDIYO. Nilibahatika, na namshukuru Mungu kwa kunipa bahati hiyo, kwamba siyo tu nilikuwa nakutana na Maalim Seif bali tumefanya kazi pamoja kufanikisha jambo moja kubwa sana katika nchi hii, jambo la MARIDHIANO yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapa Zanzibar.

"Tulianza kufanya kazi na Maalim Seif na ndugu yangu Ismail Jussa kuhusu suala hili tokea mwaka 2004. Nilipata nguvu ya kuliendea jambo hili baada ya kuwa nilishakutana na kufanya mazungumzo mara nyingi sana na rafiki yangu, Rais mstaafu Amani Karume, tangu kabla hajawa Rais, na kuweza kuona shauku yake ya kuiondoa Zanzibar kwenye siasa za migawanyiko na mifarakano. Hilo lilinivutia na nikaamua kufanya kazi naye.

"Ulipokuja uchaguzi wa 2005 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuteuliwa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungao kupitia CCM, tukaona tuna fursa nzuri ya kulifanikisha hili.

"Huu ulikuwa ndiyo msingi wa mazungumzo ya Muafaka wa Tatu ambayo yalikwaa kisiki na hatimaye yakaja kukawamuliwa na mazungumzo ya Maridhiano kati ya Rais mstaafu Amani Karume na Maalim Seif hapo mwaka 2009.

"Kamati ya Maridhiano ikaundwa Zanzibar, kura ya maoni ikafanyika, Katiba ya Zanzibar ikabadilishwa na hatimaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikaanzishwa Zanzibar.

"Nimeamua kuyasema haya ili kukumbusha tu kwamba mtu ambaye ndiye sababu ya kukusanyika kwetu hapa hakuwa mtu wa kawaida.

"Ni mtu aliyejitoa nafsi yake na akaukataa ubinafsi kwa kujali nchi yake na watu wake. Huyo ndiye Maalim Seif. Ni aina ya viongozi ambao ni nadra sana kutokea katika nchi.

"Huwa ni zawadi kutoka kwa Mungu na huchukua miaka mingi na vizazi kadhaa kabla ya kuja mwengine. Kwa nguvu ya kisiasa aliyokuwa nayo angeweza kuamrisha lolote na wafuasi wake wakatekeleza, lakini yeye mara zote alijali maslahi mapana ya nchi yake na watu wake.

Bila shaka, bila ya elimu bora kwa Wazanzibari ndoto ya Zanzibar Mpya haitaweza kufikiwa. Hata hivyo, ni imani yangu thabiti kwamba bila Umoja katika hali ya kuwepo Maridhiano hata muda wa kuwaza kuwa na ‘Zanzibar Ambition’ kama aliyokuwa nayo Maalim Seif hautakuwepo.

"Kuna ushahidi wa kisayansi kuhusu faida ya umoja na maridhiano katika maendeleo ya watu. Hapa nitanukuu matokeo ya utafiti wa kitaalamu yaliyotolewa mwaka 2017.

"Katika Taarifa iliyoitwa Zanzibar Poverty Assessment, wataalamu walionyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano (5) kati ya 2010 – 2015, kasi ya kupungua kwa umasikini ilifikia asilimia 11.

Hii ilikuwa ni kasi kubwa zaidi ya kupungua umasikini Zanzibar kuliko wakati wowote tangu mwaka 1964.

Itakumbukwa kuwa kipindi hiki ndio kipindi ambacho Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa kwa mara ya kwanza na Zanzibar kupata utulivu mkubwa; na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi zilizozalisha ajira kwa Wazanzibari na kuwapa kipato cha kuendesha maisha yao.

Nina hakika takwimu za kati ya mwaka 2015 – 2020 zitakapotoka hali itakuwa ni tofauti sana, huku ikizingatiwa pia kipindi hicho dunia ilipata janga la ugonjwa wa COVID-19.

Katika hali kama hiyo, tunaweza kufahamu kwa nini Maalim Seif alitumia maarifa, nguvu na uwezo wake wote kuhakikisha Zanzibar inakuwa moja na yenye maridhiano.

Lakini nje ya hayo, Maalim Seif pia alikuwa na dira ya namna ya kuijenga Zanzibar Mpya ambayo msingi wake ulikuwa ni Elimu. Mwenyewe akiifupisha dira yake hiyo kupitia maneno yaliyojikita kwenye dhamira aliyokuwa akiirudia mara kwa mara – dhamira ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika. Na hilo ndilo ninalotaka kujikita nalo katika mazungumzo yangu hapa leo.

Maalim Seif: Elimu, Maridhiano na Uchumi

"Waandaaji wa Mkutano huo wamenitaka nizungumzie Elimu kama nyenzo ya kukuza uchumi na kuzalisha utajiri katika nchi, huku nikifanya rejea kwenye Dira ya Maalim Seif.

Nianze kwa kunukuu sehemu ya Taarifa ya hali ya umasikini nchini Tanzania iliyotoka mwaka 2020, ambapo wataalamu walioiandaa walisema, “Tanzania inapaswa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtaji wa watu (human capital) na kuongeza ujuzi (skills) kwa nguvu kazi yake ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira hasa katika sekta zinazoongeza kasi ya ukuaji wa uchumi”.

Nukuu hii ni sahihi kwa Zanzibar kama ilivyo kwa Tanzania Bara, lakini pia ni sahihi kwa Afrika na nchi yoyote duniani. Elimu ni msingi mkubwa na muhimu sana wa maendeleo ya Taifa lolote duniani kwani takwimu zinaonyesha kuwa watu wenye elimu na ujuzi wanafanikiwa zaidi kuondoka katika dimbwi la umasikini kuliko watu ambao hawana elimu.

Maalim Seif, katika uongozi na dira yake, alisisitiza sana umuhimu wa kujenga uwezo wa kielimu kwa Wazanzibari ili kuweza kukabili changamoto za maisha yao, kuleta maendeleo yao na kutenegeneza utajiri katika nchi yao.

Alikuwa na ndoto ya kuifikisha Zanzibar mahala pakubwa kiuchumi na katika maendeleo ya jamii kwenye eneo letu la ukanda wa Afrika Mashariki na katika Dunia. Kutengeneza ndoto kwa unaowaongoza, na kuwapa hamasa na imani ya kuweza kuifikia ndoto hiyo, ni wajibu mkubwa wa kiuongozi lakini sio viongozi wote wana uwezo huo.

Jarida la Foreign Affairs, toleo la Julai/Agosti mwaka huu wa 2022, limeelezea umuhimu huu wa kuwa na ndoto ya Taifa, na naomba ninukuu:

“Katika ujenzi wa misingi ya Taifa, shabaha inayokubalika na wote au kwa nchi nyengine huita ndoto ya Taifa, ni jambo la muhimu sana.

Bila kuwa na ndoto ya Taifa, jambo ambalo kila mwananchi analipigania kwa namna yake, inakuwa vigumu sana kuwaunganisha watu pamoja na kuchochea nguvu zao katika ujenzi wa Taifa lao. Mataifa hukua au huanguka kutokana na sababu mbali mbali, lakini kukosekana kwa sifa zinazolitambulisha taifa (national character) huharakisha zaidi kuanguka kwao.”

Kama ambavyo tunajadili katika mada hii, wakati mwengine huwa tunaelekeza nguvu nyingi kwenye ukuaji wa uchumi. Ni kweli kuwa ukuaji wa uchumi ni chanzo cha nguvu ya taifa lolote. Lakini ni muhimu kusisitiza umuhimu kujenga ndoto ya Taifa (national ambition);raia wote kuwa na fursa sawa za maendeleo, kujenga utaifa, dola lenye nguvu ujenzi wa Taasisi imara.

Hili ndilo jambo ambalo Maalim alikuwa analipigania maisha yake yote – Zanzibar inayopaa kiuchumi ikiwa ni kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo la Afrika Mashariki (Singapore ya Afrika). Ndoto hii haipaswi kuachwa, bali ni wajibu wote sote kuendelea kuipigania.

Mara moja wakati tumekaa na tunabadilishana mawazo na Maalim Seif. Nikamwambia kwamba amekuwa akiwapa matumaini makubwa Wazanzibari kuwa ataweza kuwaongoza kubadilisha maisha yao ndani ya muda mfupi.

Nikamuuliza atalifanikisha vipi hilo? Jibu lake lilionesha mtu anayejua anachokitaka na vipi atakifanikisha. Alinambia, huwezi kuzuka tu na miradi, bali ni lazima kwanza uwe na dira. Akanambia yeye anayo dira ya vipi kuweza kuibadilisha Zanzibar kuwa nchi tajiri ambayo watu wake wanaishi vizuri na kupata huduma bora kutoka Serikali yao.

Lakini akasema dira hiyo haiwezi kufanikiwa ikiwa wananchi wa Zanzibar hawatakuwa sehemu yake, na badala yake wakawa watazamaji tu wa mafanikio ya wawekezaji kutoka nje.

Akasema, katika hali iliyoonesha ana imani ya dhati ya anachokisema, kwamba hakuna njia ya mkato ya kuwafanya wananchi kuwa sehemu ya dira hiyo na kunufaika nayo, zaidi ya kuwekeza kwenye elimu bora na ya kisasa inayojielekeza kwenye fikra huru (critical thinking), maarifa makubwa na weledi, ubunifu na kujenga watu wanaojiamini. He couldn’t be more right. Mtazamo wake ulikuwa sahihi kabisa.

Ni vipi basi elimu inaweza kuwa nyenzo ya ukuzaji uchumi na utengenezaji wa utajiri kwa nchi na watu wake?.

Kwa mtazamo wangu, elimu inaweza tu kuwa mkombozi wa watu ikiwa itakuwa ni elimu bora inayojikita kuwajengea watu uwezo wa kutambua fursa zilizopo mbele yao, vipi wazitumie fursa hizo, na vipi wafaidike kutokana na fursa hizo.

Hivyo basi, elimu yetu inapaswa kuwafanya wahitimu wetu wawe watu wenye uthubutu wa kuhoji na kujihoji (critical thinking), iwafanye wahitimu wetu wawe watu wanaoweza kujitathmini (self-assessment and self-evaluation), iwafanye wahitimu wetu wawe na kiu isiyokwisha ya kujiongezea maarifa mapya katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kila uchao (thirst of acquiring new knowledge and skills), iwafanye wahitimu wetu wawe watundu na wabunifu (innovative and creative), na iwafanye wahitimu wetu wawe na uthubutu na wanaojiamini (daring and self-confident).

Wakati umefika wa kuondokana na mfumo wa elimu ya kikoloni uliolenga kutuzalishia watumishi watiifu na waaminifu kwa mamlaka zao (Your most loyal and obedient servants).

Hakuna ubishi kwamba Elimu ni muhimu katika kufikia maendeleo ya mtu binafsi na maendeleo ya nchi. La kujadiliana hapa ni aina ya elimu tunayotoa.

Umuhimu wa elimu katika maendeleo ya watu na nchi umethibitishwa kisayansi kabisa. Takwimu zinatuonyesha kuwa familia za Wazanzibari ambazo wakuu wa familia wana angalau elimu ya sekondari hali zao ni bora zaidi kuliko familia ambazo wakuu wa familia wana elimu chini ya kidato cha nne au hawana elimu kabisa. Elimu ndio mtaji wa umma.

Elimu ni moyo wa Maendeleo ya Taifa lolote maana inawezesha nchi kupata teknolojia za kisasa na kujenga uwezo wa kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya maana yanayobadilisha Maisha ya watu. Elimu bora huzalisha utajiri wa taifa (wealth creation) ambao hutumika kuwekeza zaidi kuongeza kasi ya maendeleo.

Hali ya Elimu kwa Zanzibar ina nafuu kulinganisha na nchi nyengine za kusini mwa jangwa la Sahara, kwa maana ya idadi ya wanaopata nafasi lakini tatizo kubwa linabaki kuwa ni kiwango cha elimu inayotolewa.

Nusu ya Wazanzibari angalau wana elimu ya sekondari na ni asilimia 20 tu ya Wazanzibari ndio hawana elimu ya aina yeyote. Hata hivyo kilio kikubwa ni ubora wa elimu inayotolewa kwa Wazanzibari.

Katika kumuenzi Maalim Seif, ni muhimu sana kuwekeza nguvu kubwa katika ubora wa elimu ili kuwaandaa Wazanzibari kwa uchumi ambao yeye Maalim Seif akiamini unapaswa kufikiwa – ambao ni wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika -Kituo cha Biashara na Huduma katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.

Kwa kuwa Dira ya Maalim Seif na Wazanzibari wengi ni Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika, ni vyema kutazama namna nchi hiyo ilivyoweka nguvu kwenye elimu katika maendeleo yake.

Waziri Tharman Shanmugaratnam wa Singapore amenukuliwa katika Kitabu cha The Asian Aspiration akisema “Elimu ndio mkakati wetu muhimu zaidi kiuchumi na kijamii. Tangu tumepata Uhuru tuliamua kuondoa siasa kwenye elimu lakini tulichukua maamuzi ya kisiasa kuhakikisha kuwa elimu yetu inazingatia matokeo bora ya kusukuma nchi mbele. Vile vile tulizipa mamlaka za elimu uhuru mkubwa”.

Hivi karibuni tu, kuna video moja imekuwa ikizungushwa sana kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha Waziri Mkuu Lee Hsien Loong wa Singapore akisema kwamba sera ya Singapore ni kuvutia watu wenye vipaji vikubwa vya elimu (wale ambao sisi tunawaita akili kubwa) wahamie na wabakie Singapore.

Alisema hao wanaweza kuwa chachu ya maendeleo ya Singapore. Mbegu ya kuthamini elimu na weledi katika kuijenga Singapore mpya iliyo tajiri imeelezwa kwa ufasaha zaidi na Waziri Mkuu wa mwanzo wa Singapore, Lee Kuan Yew, katika kitabu chake cha The Singapore Story: From Third World to First, ambapo alisema waliwekeza nguvu kubwa katika kuinua kiwango cha elimu nchini humo kwa sababu waliamini kuwa elimu ndiyo itakayoijenga Singapore aliyokuwa akitaka kuiona.

Lakini kutoa elimu hakukutosha. Akasema katika kuajiri waliondosha upendeleo wa aina zote na badala yake wakenda kujifunza na kuutumia mfumo wa kampuni kubwa ya biashara ya mafuta ya Shell inayotajika kwa mafanikio duniani katika kuajiri ambayo inaangalia sifa za mtu (meritocracy) – mkazo ukiwa ni uwezo, vipaji na weledi.

Hivyo ndivyo Singapore ilivyojengwa. Na hivyo ndivyo mfumo wa elimu katika nchi yoyote iliyodhamiria kufikia ukuaji mkubwa wa uchumi na kuzalisha utajiri wa taifa unavyopaswa kuwa. Msingi wa mfumo wa elimu kama huo unapaswa kuwa uhuru wa mawazo (freedom of thought au critical thiking), ubunifu (innovation) na uwezeshaji (empowerment), ambayo nafurahi kuona kuwa ndiyo maudhui ya Mkutano huu.

Utafiti wa viwango vya elimu katika nchi 54 za Afrika ukiofanyika mwaka jana umebainisha kwamba Seychelles na Mauritius, nchi za visiwa kama Zanzibar, zinashika nafasi ya kwanza na ya tatu kwa ubora wa elimu wanayotoa. Kama Seychelles na Mauritius wameweza, Zanzibar pia inaweza.

Katika kumuenzi Maalim Seif, Zanzibar inapaswa sasa kupanga mpango wa muda mrefu wa elimu inayopaswa kuendesha uchumi inaoutaka. Kwa Zanzibar pa kuanzia papo.

Pa kuanzia ni wapi? Zanzibar ina Wazanzibari wengi waliopo nje (diaspora) waliokwenda kutafuta maisha na hivyo kupata elimu kubwa. Inapaswa kuwa sera mahsusi kuwavutia kurudi kwa ajili ya kujenga mfumo madhubuti ambao utahakikisha kizazi kipya cha Wazanzibari kinatayarishwa kuwa na elimu inayokidhi maendeleo ya dunia ya sasa na ndoto ya aina ya uchumi ambao Zanzibar inataka kuujenga.

Kiwango cha Wazanzibari wenye elimu ya Sekondari ni kikubwa kuliko nchi yeyote ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, hivyo kinachotakiwa ni kujenga uwezo wao hawa (re-education) kwa kupitia njia mbali mbali zitakazopaswa kubuniwa na kuongeza kiwango cha ujuzi (skills).

Elimu inayotoa ujuzi itasaidia kujenga mtaji wa umma wa ndani ili kuwezesha wananchi wa Zanzibar na Tanzania kufaidika kwa pamoja na juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, katika kuchochea mitaji kutoka nje.

Ni muhimu hapa niweke msisitizo mkubwa kwamba mitaji kutoka nje (FDI) ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwani mitaji hii inaziba pengo la uwezo wetu mdogo wa kuweka akiba tulio nao sasa

Uwiano wa uwekaji akiba kwa Pato la Taifa (savings-GDP ratio) hapa Tanzania ni wa kiwango cha chini sana, chini ya asilimia 15, wakati kwa uchumi wetu na ili tupige hatua kubwa ya maendeleo tunahitaji angalau uwiano wa 30%. Hii nakisi inafidiwa na akiba za watu wengi kutoka nje.

Tangu ameingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan na vile vile Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa mstari wa mbele kushawishi mitaji kutoka nje kuingia nchini.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Machi 2021 mpaka Machi 2022, Mitaji kutoka nje iliyoingia nchini iliongezeka kwa 300% kutoka USD 1.13 bilioni mpaka USD 4.144 bilioni.

Vile vile kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeweza kufungua mahusiano yake na mashirika ya kimataifa kiasi cha kufaidika na mikopo nafuu ya riba sifuri kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo fedha hizo zilielekezwa katika uwekezaji katika sekta za elimu na afya.

Uwekezaji wa kiwango hiki pamoja na faida zake zote hautakuwa na tija kubwa, iwapo Watanzania hawaandaliwi kuwa na elimu yenye ujuzi; na matokeo yake watashindwa kutumia fursa ipasavyo na faida yote kwenda kwa wawekezaji kutoka nje na kuwafanya Watanzania na Wazanzibari kubaki watazamaji tu. Hii ni hatari kwa taifa lolote lile.

Juhudi zinazofanyika sasa za Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi kutazama sekta ya Elimu Zanzibar kwa kuunda Kikosi Maalum kilichosheheni wataalamu wabobezi wa Elimu kwa lengo la kuona namna ya kuongeza ubora wa Elimu Zanzibar ni juhudi zinazopaswa kuungwa mkono na ni njia bora ya kumuenzi Maalim Seif.

Lakini kama nilivyosema, elimu bila ya umoja na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari haitotufikisha popote.

Bahati nzuri, kwa jinsi ninavyomfahamu Dk. Hussein Mwinyi ni muumini wa maridhiano, na kwa kuwa anajali maendeleo ya Wazanzibari na kwa sababu anajua hayawezi kupatikana bila maridhiano basi naamini tutaona Maridhiano yanaimarika zaidi.

Maendeleo ya kiuchumi na hususan uimarishaji wa uchumi mpana kinapaswa kuwa kipaumbele cha Serikali yeyote ile iliyo makini kwani kukua kwa shughuli za uchumi ndio kunazalisha ajira na hatimaye maisha ya wananchi kuwa mazuri na bora zaidi.

Ninaweza kutamka kwa ushahidi wa kisayansi kuwa katika historia fupi ya nchi yetu tangu Uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania, kila Jamhuri yetu inapopata viongozi wakuu kutoka Zanzibar kumekuwa na mafanikio makubwa ya mageuzi ya kiuchumi.

Tuliona hivyo wakati wa uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi na tunaona hivyo hivi sasa wakati wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ni dhahiri hii inatokana na ukweli kuwa Zanzibar ina historia ndefu yenye mkusanyiko wa watu kutoka kila pembe ya dunia, yaani metropolitan na imejenga misingi ya biashara na kutoogopa ushindani. Matokeo yake ni fursa na mzunguko wa fedha kuongezeka, na uchumi kuimarika.

Maalim Seif, licha ya kwamba hakuwahi kuwa Kiongozi Mkuu wa nchi yetu, lakini katika wadhifa alioshika Serikalini alionyesha juhudi za ujenzi wa Uchumi.

Alipokuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Mipango na Uchumi miaka ya themanini, katikati ya utaifishaji wa mali za watu, Maalim alizuia baadhi ya utaifishaji kwa sababu tu aliamini kuwa uchumi unajengwa na sekta binafsi.

Maalim Seif anahadithia mwenyewe kuwa alipotembelea kiwanda cha kuchakata mafuta ya kula cha Rajani kule Shinyanga na kukutana na wamiliki na kuelezwa namna biashara ile inafanya kazi, alizuia utaifishaji wa kiwanda kile.

Hata Sera za kufungua milango ya biashara ambazo Rais Mwinyi alifanya baada ya mwaka 1985 zilitokana na kazi ambayo Maalim Seif alifanya na Rais Mwinyi wakati wawili hao wakiendesha Serikali ya Zanzibar mwaka 1984.

Hakika Maalim Seif alikuwa miongoni mwa viongozi mahiri wenye maono, dira na nia ya kuipeleka Zanzibar na Tanzania katika uchumi wa juu zaidi kwa manufaa ya watu wake.

Nirudie kusisitiza kuwa Uchumi endelevu ni uchumi ambao unashirikisha wananchi vya kutosha. Wananchi hawawezi, na hawapaswi kuwa watazamaji tu au wafanyakazi tu wa wageni.

Ni lazima elimu na juhudi za makusudi za kisera zielekezwe kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika uchumi. Tusibaki kufurahia takwimu tu za ongezeko la mitaji, kukua kwa GDP n.k. Kama watu hawaoni mabadiliko, hizo takwimu hazitakuwa na msaada wowote.

Hapa Zanzibar, wananchi wengi wapo katika sekta ya huduma kwa sababu ya aina ya uchumi wake. Ni lazima mfumo wa elimu Zanzibar uhakikishe kuwa Wazanzibari wanakuwa na ujuzi wa kutosha kushiriki katika sekta kuu ya Utalii lakini pia sekta zinazounganika na sekta hiyo kama vile sekta ya huduma za usafiri wa baharini, angani na nchi kavu, huduma za fedha na mabenki, uhasibu, ukaguzi, uanasheria, uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika katika Utalii zikiwemo zinazotokana na kilimo cha mboga mboga na matunda, ufugaji na uvuvi, uendeshaji wa mikahawa ya kisasa, na biashara za vito vya thamani.

Zanzibar sio tu itoe wafanyakazi wazuri wa mahoteli bali pia itoe mameneja bora na wabunifu wanaoweza kusimama na kuhesabika katika huduma zote muhimu zinazoendesha uchumi wa visiwa hivi.

Sekta mpya zinazoibuka Zanzibar ni pamoja na Gesi Asilia na Mafuta, Nishati inayotokana na vyanzo visivyomalizika kama jua na upepo (renewables) na kilimo cha matunda, viungo (ambapo hapa Zanzibar kumekuwa na uzalishaji wa muda mrefu wa kienyeji) na mboga mboga.

Uzalishaji wa viungo na mboga mboga unahusiana moja kwa moja na ukuaji wa sekta ya Utalii. Zanzibar leo inapokea watalii chini ya 600,000 kwa mwaka na tayari tunaona sehemu kubwa ya vyakula hata mboga mboga vikiagizwa kutoka nje ya Zanzibar.

Hivi wakifika watalii milioni 2 kwa mwaka tutajenga terminal ya kuingiza mchicha, nyanya, vitunguu n.k. pale Bandarini? Ni vema sasa hatua mahsusi zichukuliwe kuwajengea uwezo wa elimu Wazanzibari ili wawe na ujuzi wa kuzalisha kwa tija bidhaa hizi ndani ya ardhi ya Zanzibar.

Ili hoja yangu ieleweke vizuri ni vyema nikatoa mfano wa vipi elimu na maarifa huleta mabadiliko, kukuza uchumi na kutengeneza utajiri. Mfano huu unahusu sekta ya kilimo ambao ndio husahaulika sana. Huwa napenda kuutoa kule Tanzania Bara.

Hivi tunajua kuwa mkulima wa tumbaku wa Zimbabwe, mathalan, huvuna majani ya tumbaku mara tano zaidi katika kila ekari ukilinganisha na kinachovunwa katika ekari ya mkulima wa Tanzania? Tija hii inatokana na utaalamu ambao ni zao la elimu ya mara kwa mara.

Kwenye chai ni hivyo hivyo, Tanzania yenye mashamba ya chai ekari mara 3 zaidi ya Sri Lanka hupata mapato ya fedha za kigeni kiasi cha USD milioni 34 tu kwa mwaka wakati Sri Lanka hupata mpaka USD milioni 900 kwa mwaka.

Hadithi ni hiyo hiyo kwenye karafuu ukilinganisha Zanzibar na nchi nyengine zinazolima zao hilo na hata mwani. Ni lazima tubadilishe mfumo wetu wa elimu tunayotoa kwa watu wetu ili ujibu changamoto hizi.

Ni muhimu sana kutoa ujuzi wa kutosha wa mara kwa mara kwa watu wetu. Tuondokane na elimu ya kukaririshwa, twende kwenye elimu inayofikirisha na kutoa majawabu ya changamoto zetu – elimu itakayokuza uchumi wetu na kutengeneza utajiri wa taifa na watu wake.

Kwa upande wa Mafuta na Gesi Asilia, Nishati inayotokana na vyanzo vya jua na upepo na maeneo ya usafiri wa baharini na angani ni muhimu zaidi kuwaandaa vijana wetu katika ngazi zote za ujuzi zinazotakiwa. Elimu itukomboe tusiwe, watazamaji katika jitihada za kukua kwa uchumi. Watunga sera wetu walikumbuke hili muda wote.

Tukiweka nguvu ya kutosha kwenye kubadilisha na kuimarisha mifumo yetu ya elimu na kuimarisha umoja wa Wazanzibari kwa kujenga katika msingi uliopo sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar itaweza kujenga Uchumi wake kwa kutumia fursa yake ya kijiografia katika eneo hili la Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Bahari ya Hindi.

Bila ya Elimu na Mshikamano wa Kitaifa itakuwa ni vigumu sana kukuza uchumi na kuzalisha utajiri wa taifa.

Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo yake na Rais William Ruto wa Kenya hivi karibuni, tusipoimarisha uwezo wa watu wetu kushiriki katika uchumi, tutajikuta tunagawana umasikini badala ya kugawana utajiri.

Ni kwa sababu watu wetu hawana elimu na ujuzi, ndiyo maana tunapata “wawekezaji” uchwara ambao wanakuja kuchukua fursa za Watanzania mithili ya mtu anayeona kwa mbali ameingia kwenye eneo la watu vipofu.

Kwa kulitambua hilo, ndiyo maana Rais Samia amejitoa na kujipambanua kuwa mkombozi halisi wa wanyonge na masikini wan chi hii, kwa tafsiri sahihi ya neno hili. Mtetezi au mkombozi wa wanyonge si anayepiga piga kelele kusema bali ni yule anayewapa vituo vya afya, kuwajengea shule, kuwajengea masoko, kuwafungulia fursa za biashara na ujasiriamali na kuifungua Tanzania kimataifa ili kuongeza fursa kwa Watanzania.

Unaiona dhamira yake hasa ya kuwafanya Watanzania wawe wachezaji, na siyo watazamaji tu wa maendeleo ya wengine. Anataka kuona Watanzania kuwa washiriki na siyo waimba mapambio.

Utajiri unatengenezwa kwa uchumi kukua kwa kasi kubwa ukishirikisha watu (local participation). Ili uchumi ukue kwa kasi kubwa na ushiriki wake uwe mpana ni lazima watu wawe na maarifa ya kutosha kuendesha uchumi huo.

Maalim Seif alitaka kujenga Zanzibar yenye watu wenye elimu na maarifa ya kutosha kuendesha uchumi ambao unatoa huduma kwa eneo lote la Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Bahari ya Hindi. Kuiishi dira yake, tunapaswa kujielekeza huko. Hiyo ndio namna bora kabisa ya kumuenzi Mzee wetu huyu.

Kwa mtazamo wangu, na nina hakika tukitafakari vizuri tutakubaliana sote, kuwa viongozi wa aina ya Maalim Seif ndio wanaofaa kutuongoza ili maisha yetu yawe mazuri zaidi na yawe bora zaidi.

Kila leo yetu iwe bora zaidi kuliko jana yetu, na kila kesho yetu iwe bora zaidi kuliko leo yetu. Watoto wetu wapate elimu, vijana wetu wapate ajira, mama zetu waweze kuishi maisha bora bila ya kuhangaika na kuteseka na wajasiriamali wetu waweze kutajirika na kutengeneza mitaji ya kuwekeza zaidi. Ni muhimu kuwaenzi viongozi wa aina ya Maalim Seif.

Nimefurahi kusikia kuwa Zanzibar mmeunda Kikosi Kazi cha kuangalia namna ya kufanya mageuzi makubwa ya mfumo wa elimu.

Wito wangu kwa watunga sera na wenye mamlaka ni kutofanya mageuzi ya juu juu tu, bali ikibidi hata kufanya Mapinduzi ya mfumo wa elimu ili ukidhi mahitaji ya Zanzibar ya sasa na kizazi kipya.

Kikosi kazi cha Elimu Zanzibar kisiangalie tu upungufu wa majengo na vifaa, bali kiagalie walimu wetu na jinsi wanavyopatikana, maslahi yao ili kuwapa motisha lakini kubwa na muhimu kuliko yote kuiangalia kwa kina mitaala na mitindo ya usomeshaji wa vijana wetu na kuibadilisha ili ikidhi mahitaji ya kutupa elimu inayofikirisha, elimu inayokuza ubunifu na elimu inayowawezesha vijana wetu kuwa uthubutu.

Kutokana na udogo wake, Zanzibar inaweza kutuonesha njia, na inapaswa kutuonesha njia kama zilivyofanya Singapore na Mauritius. Tunataka tuisome Zanzibar ikiwa miongoni mwa nchi 3 bora kwa kiwango cha elimu katika Afrika. Na hilo linawezekana.

Nimalizie kwa kuacha swali kwa washiriki wa Mkutano huu mkubwa na muhimu. Kwa muda mrefu tumekuwa tukigubikwa na mjadala usioisha wa Muundo wa Muungano ambao unaipa Zanzibar nafasi yake ya kukuza uchumi kama nchi nyingine zenye uchumi wa visiwa. Sitaki kuingia kwenye muundo kisiasa maana najua mjadala hautakiwsha.

"Swali langu linahusu muundo kiuchumi. Ni kwa nini hatujadili kwa kutazama mahusiano ya kiuchumi kati ya China na Hong Kong katika kuitazama Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano? Historia inatufunza nini katoka Guangzhou, China na namna zoezi lile lilivyobadili Uchumi wa China?

"Hebu tutafakari haya. Sio dhamira yangu kubadili msemo wa Rais Kwame Nkrumah kwamba tafuta kwanza uhuru wa kisiasa na mengine yote yatafuata. Lakini, inawezekana sasa tuanze kutazama namna ya kupata masuluhisho ya masuala ya kisiasa kwa ‘Seek ye the economic freedom,"amefafanua Rostam Aziz.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Sijacjoka kuisoma hii , Rozstam his brilliant and very bright person on Earth! He deserve to be such a rich.
    Natamani nipate wasaa wa nusu saa tu kubadirishana naye mawazo

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news