BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 43

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... tulimsogelea tukamwagia dawa ya wijaa, kisha tukaanza kumshughulikia. Tukiwa kwenye mchakato wa kumshughulikia ghafla mlango ulifunguliwa wakaingia wachina wanne, mikononi walikuwa wameshika vyema bastola...

Endelea

Tukajibadili katika umbo la mbu wadogo zaidi, lengo letu ilikuwa ni kujificha dhidi ya wachina hao. Tayari mwenzetu alikuwa ameshapoteza uhai kupitia bastola ya yule mchina, kwa namna moja au nyingine tulipaswa kuwa makini katika vita hiyo. Wakati huo tulikuwa tumening'inia ukutani kama mbu wafanyavyo. 
Ulitakiwa kuwa na macho ya pili kugundua kuwa wale hawakuwa mbu bali binadamu. Ndugu msomaji mara nyingi wachawi wamekuwa wakiingia majumbani kwenu kupitia maumbo mbalimbali. Si rahisi kuwaona wachawi kadri unavyojisikia.

Wachawi wanapohisi hatari fulani wawapo kwenye mji wa mtu huchukua tahadhari kubwa. Miongoni mwa tahadhari hizo ni pamoja na kuchukua maumbo ya aina mbalimbali. 

Japokuwa ni vigumu kuwaona katika macho ya kawaida, lakini huwa kuna muda anaweza kuonekana. Mchawi anaweza kuonekana rahisi kupitia njia mbalimbali, njia ya kwanza ni pale anapoamua kukutisha. 

Mchezo huu hufanywa na wachawi aina ya wanga, lengo lao ni kufurahia tabu atakayopitia mtu huyo. Lengo la pili ni kukamilisha masharti ya madawa, ambayo humtaka kufanya hivyo kama sehemu ya tambiko la madawa yake. 

Anaweza kuchukua umbo lake kamili lakini akaweka kichwa cha kiumbe mwingine, lengo lao ni kukuona unahangaika ndipo wao hafurahi. Mara nyingi wachawi wa namna hii hufanya shughuli zao mapema sana kabla ya usiku wa manane.

Njia nyingine ya kumuona mchawi kirahisi ni pale anapokutembelea nyumbani usiku. Ndugu msomaji inapotokea ghafla unatoka kwenye usingizi ukahisi mwili kusisimukwa huku nywele zikiwa zimesimama tambua kuna mchawi amekuja kukutembelea usiku huo. 

Ili umuone kirahisi pasipo hata kutumia dawa. Toka ndani ukiwa uchi wa mnyama, hakikisha hauchukui kitu cha aina yeyote. Ukitoka nje utakuta akiwa katika umbo la kawaida la kibinadamu, inahitaji sana uvumilivu endapo watakuwa wengi wanaweza kushirikiana kukupiga mpaka kufa. Ila kama atakuwa pekee unaweza kupambana naye mpaka ukamshinda, katika hili jiandae kuishi kwa shida katika maisha yako yote.

Njia nyingine ya kuwaona wachawi, baadhi ya watu katika miili yao wana nguvu za ziada. Watu hao wamezaliwa wakiwa hivyo toka tumboni mwa mama zao. 

Ni vigumu kuwachukua misukule, watu wa aina hii huwa na nguvu za kutisha ndani ya miili yao. Mara nyingi sisi wachawi huwa tunawatambua kupitia joto la miili yao, pindi unapomsogelea mtu huyo huwa wana joto kali mithili ya tanuru la kuchomea tofari. Watu hawa huwa na uwezo wa kuwaona wachawi kirahisi, kulingana na maumbile yao ni wagumu sana katika kuogopa.

Njia nyingine ni ile ya kutumia madawa, hii huitaji nguvu za madawa ya kutosha. Wachawi wengi pamoja na waganga ndiyo hutumia njia hii, huhitajika madawa ya kutosha katika kuwaona wachawi wakiwa kwenye shughuli zao. Hii ndiyo njia aliyoitumia yule mchina kumuua mwenzetu kwa risasi, kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kumuona ndiyo maana alimpiga risasi iliyokuwa imepakwa dawa za kutosha.

Tukiwa tumening'inia ukutani katika umbo la mbu, tulibaini wachina hao wanne walikuwa hawatuoni. Mle chumbani walimkuta mwenzao yuko hoi bin taabani, maana tulikuwa tumeshaanza kumwagia madawa ya kumfanya kuwa msukule. 

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na maiti ya mchawi mwenzetu, damu zilikuwa zimetapakaa chumbani humo mithili ya ziwa dogo. Risasi aliyopigwa na mchina huyo iliingia kifuani kisha ikafumua nyuma ya mgongo na kumfanya nyang'anyang'a. Wale wachina walionekana kupigwa butwaa, bastola zilikuwa mikononi mwao tayari kwa lolote lile.

Tulikuwa tumeshagundua kuwa wachina hao walikuwa hawatuoni, tulipaswa kutumia mwanya huo kuwabana ili iwe faida kwetu. Miongoni mwao wachina wawili walifungua mlango na kutoka nje, kisha wakabaki wachina wawili chumbani humo pamoja na yule aliyekuwa hoi kitandani akawa wa tatu. 

Tukautumia muda huo kuwakaba wale wawili waliobakia chumbani humo na yule wa tatu, tukafanikiwa kuwabadili katika hali tuliyotaka. Tuliwanyemelea tena wale wale wawili waliokuwa nje, bila usumbufu tukafanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi. 

Kule nje karibu na migomba tulihakikisha lile shimo walimokuwa wakihifadhi miili ya binadamu baada ya kuwaua panabaki wazi. Lengo letu ilikuwa ni kuwaonesha mamlaka nyuma ya pazia kinachofanywa na baadhi ya wachina wasio waungwana.

Tulirudi vyumbani kwa wachina hao tukiwa na magogo ya migomba, magogo hayo tulikuwa tumeyatoa nje ya eneo hilo la kempu ya Wachina. Tuliyafanyia taratibu zote za kichawi kisha tukachukua picha za wachina hao tukazivalisha kwenye migomba hiyo. 

Tulichukua migomba hiyo tukailaza kwenye vyumba walivyokuwa wakilala wachina hao. Lengo letu ilikuwa ni kuondoa sintofahamu lakini pia kukamilisha taratibu za kichawi. 

Baada ya hapo tuliondoka na wachina hao ambao walionekana kama zuzu kulingana na madawa tuliyokuwa tumewapulizia. Tulikwenda mpaka uwanja wa shule ya msingi Nyambutwe tulipokuwa tumeacha nyungo zetu.

Kabla ya kupanda ungo, nilipiga makofi mawili huku nikinuia jambo. Baada ya sekunde kumi kilikuja kimbunga kikubwa, nilikituliza kisha tukawapandisha wachina hao kisha tukakiruhusu kuondoka nao. 

Huu ulikuwa usafiri maalumu kwa ajili ya kusafirisha watu wa namna hiyo, upepo uliwabeba misukule hao wa kichina kisha wakasafirishwa kwenda kwenye kambi yetu ya misukule. Tukapanda kwenye nyungo zetu kisha tukaelekea kambini, punde si punde tulifika kambini sambamba na wale misukule wa kichina.

Lilipita juma moja tukiwa kwenye maandalizi ya ujenzi wa *GAMBOSHI MPYA*, maandalizi ya ujenzi yalikuwa yakienda vyema. Vifaa vyote vya ujenzi vilikuwa eneo husika, saruji nyingi tulizipata viwandani na zingine tulizipata kwa kuangusha magari yaliyokuwa yakisafirisha kupeleka Kigoma. Mazindiko ya kutosha yalikuwa yamewekwa kwenye eneo la ujenzi, wale Wachina tayari tulikuwa tumeshawaweka sawa kwa kazi iliyokuwa mbele yao.

Ndugu msomaji usiache kufuatilia kisa hiki cha kusisimua, tafadhali ungana na mimi sehemu inayofuata

KOLAKOLA

THE BOMBOM

Ukitaka kupata sehemu ya 1 hadi ya 40 usisite kuwasiliana nasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news