Wazee epukeni kukaa vikundi na vijana vijiweni asema Goranga huku DC Kolimba akitoa msisitizo

NA SOPHIA FUNDI

VIONGOZI wa serikali kutoka ngazi zote wametakiwa kushirikiana na mabaraza ya wazee kutatua migogoro mbalimbali ya jamii hasa migogoro ya ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee yaliyofanyika katika viwanja vya Mazingira bora wilayani hapa.

Kolimba alisema kuwa, kumekuwa na migogoro mingi ndani ya jamii hasa ya ardhi ambapo watoto hugombania ardhi ya wazazi wao hadi kuwashtaki wazee jambo ambalo limekuwa likiwafanya wazazi kuishi maisha ya shida na kukosa watetezi.
"Mimi katika ofisi yangu nimetenga siku ya kusikiliza kero za wananchi, lakini utakuta malalamiko mengi ni ya wazazi na watoto wao kuhusu ardhi, hivyo nawaagiza viongozi wa serikali katika maeneo yenu shirikianeni na mabaraza ya wazee kutatua migogoro hiyo,kwani wazee ni hazina tuwalee na tuwatuze,"amesema Kolimba.

Amesema kuwa, kumekuwa na matukio mbalimbali katika wilaya ya watu kujinyonga,ubakaji na mengine mengi, hivyo mabaraza hayo yasaidie kupata chanzo na kuweza kutatua kama wazee walivyosaidia kulimaliza matukio ya fisi mla watu katika baadhi ya vijiji wilayani hapa.
"Kuna matukio mengi katika wilaya yakiwemo ya ubakaji,watu kujinyonga na mengine mengi wazee nendeni mkayatatue kama mlivyoweza kulitatua tatizo la fisi mla watu katika wilaya yetu,tafuteni chanzo ni nini na mlifanyie kazi,"alisema Kolimba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Karatu, Charles Goranga aliwaomba wazee kuepuka kukaa kwenye makundi ya vijana ili wapatiwe heshima na vijana.
"Serikali imerudisha heshima ya wazee kwa kuundwa kwa mabaraza haya ya wazee ngazi zote,hivyo wazee epukeni kukaa vikundi na vijana,utamkuta mzee yuko katikati ya vijana wanataniana utaheshimiwa kweli katika maamuzi yoyote ya kutatua migogoro? Acheni kukaa na vijana kwenye vijiwe,"alisema Goranga.

Alisema kuwa, bado kuna baadhi ya viongozi wa vijiji na kata hawashirikishi mabaraza haya kwenye vikao vya maamuzi katika maeneo yao hivyo ameomba Serikali kuingilia kati suala hilo

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news