Burundi wafika Tanzania kujifunza usimamizi Sekta ya Madini

NA TITO MSELEM

WIZARA ya Madini imepokea ugeni kutoka Jamhuri ya Burundi ikiwa ni matokeo ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi katika Sekta ya Madini.
Kufuatia kusainiwa kwa makubaliano hayo, ujumbe kutoka Burundi umekuja nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza namna bora ya kusimamia rasilimali madini.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na jiolojia ya Tanzania na jiolojia ya Burundi, uhusiano wa jiolojia ya Tanzania na jiolojia ya Burundi na majukumu ya wizara katika kusimamia Sekta ya Madini.
Aidha, ujumbe huo umefahamishwa kuhusu masuala ya uongezaji thamani madini, ushirikishwaji wa wazawa katika uchumi wa madini.

Pia, ujumbe huo, umepatiwa elimu kuhusiana na maandalizi ya Kufunga Migodi (Mining Closure), upatikanaji wa leseni pamoja na aina za leseni zinazotolewa nchini Tanzania.
Akiwasilisha mada Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka washiriki kujifunza kwa weledi mbinu bora za usimamizi wa Sekta ya Madini na kuuliza maswali yatakayo wasaidia kuboresha usimamizi wa sekta hiyo nchini kwao.
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi umeongozwa na Mshauri wa Rais katika Sekta ya Madini wa Burundi Alphonsia Kwizera ambao wamepata fursa ya kutembelea migodi mbalimbali ya wachimbaji wadogo mkoani Dodoma pamoja na mgodi wa kati wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Shanta Singida.
Tanzania na Burundi zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika usimamizi wa rasilimali madini baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan kufanya ziara nchini Burundi ambapo utekelezaji wake umeanza kufanyika kwa lengo la kuzinufaisha nchi hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news