DC Mkasaba:Serikali chini ya Rais Dkt.Mwinyi itaendelea kuheshimu na kuthamini mchango wa walimu

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi inathamini jitihada kubwa zinazofanywa na walimu nchini na ndio maana imewapandishia kiwango cha mishahara ili kuwapa hamasa na kuwasaidia katika kuendeleza maisha yao sambamba na kuleta matokea chanya kwa wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kufanya mitihani yao mwezi ujao katika Skuli ya Sekondari ya Jambiani.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba katika Mahafali ya Nne ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kufanya mitihani yao mwezi ujao katika Skuli ya Sekondari ya Jambiani iliyopo Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini aliahidi kwamba Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake ili sekta ya elimu nchini izidi kuimarika pamoja na kuwa na mazingira bora ya kufanyakazi kwa walimu wake.

Aliwasihi walimu wa Skuli ya Sekondari Jambiani kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili skuli hiyo iendelee kutoa wahitimu wenye uwezo wa hali ya juu kitaaluma na kuondokana na ile dhana ya kwamba skuli za wilaya hiyo zimekuwa hazifanyi vizuri katika mitihani ya Taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba akisalimia na Mbunge wa Jimbo la Paje, Mheshimiwa Jafar Sanya Jussa wakati wakati wa hafla ya mahafali ya watahiniwa wa Kidato cha Nne katika Skuli ya Jambiani wilayani humo.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini ameeleza juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika ikiwa ni pamoja na kutoa fedha nyingi kupitia fedha za UVIKO -19 katika ujenzi wa skuli mpya za kisasa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum na shukurani kwa wale wote wanaoendelea kuiunga mkono skuli hiyo kwa lengo la kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika katika wilaya hiyo.

Mkasaba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msaada wa chakula yakiwemo magunia 10 ya mchele, vyakula vyingine, vifaa na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wanaokaa kambi wakijiandaa na mitihani katika skuli zote za sekondari za wilaya hiyo.
Mwanafunzi mwenye mahitaji maalum ya uoni wa macho, Fadhil Murid Rajab akionesha kipaji chake katika mahafali hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Rajab Yusuf Mkasaba (hayupo pichani).

Pia, aliwakumbusha wanafunzi ambao wanajitayarisha na mitihani ya Kidato cha Nne ambao wameagwa rasmi katika hafla hiyo kutambua kwamba kumaliza kwao ngazi waliofikia ya taaluma ni mwanzo wa ngazi inayofuata.

“Wazee walisema elimu haina mwisho, kwa hivyo mnapaswa kujiandaa kwa ngazi ya taaluma inayofuata,”amesema Mheshimiwa Mkasaba.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba (wa tatu kutoka kulia) akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kada maalum ya michezo katika Skuli ya Sekondari ya Jambiani wakati wa hafla ya mahafali hayo. Skuli hiyo ndiyo pekee katika mkoa inayofundisha kada hiyo.

Sambamba na hayo, aliwasihi wanafunzi wanaoendelea na masomo yao katika skuli hiyo ya Sekondari Jambiani kuwa na bidii katika masomo na kujifunza siri za mafanikio ambayo wameyapata ndugu zao wanaotarajia kufanya mitihani yao ya Kidato cha Nne mwezi ujao.

Akieleza hatua zilizochukuliwa na wilaya hiyo katika kupambana na changamoto zilizoelezwa na wanafunzi hao katika risala yao ikiwemo suala zima la upigaji ngoma na miziki alitoa ufafanuzi juu ya kadhia hiyo alieleza kwamba tayari ofisi yake imeazimia kuwakumbusha wamiliki wote wa hoteli pamoja na baa za wilaya hiyo kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASSFU).

Pia alisisitiza kwamba kwa kipindi hichi chote ambacho wanafunzi wanajiadaa na mitihani yao ikiwemo ya darasa na Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili pamoja na Kidato cha Nne hairuhusiwi kupigwa ngoma ya aina yoyote katika hafla zote mpaka pale mitihani itakapomalizika.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo baadhi ya walimu wa Skuli ya Sekondari ya Jambiani wakati wa hafla ya mahafali hayo.

Nao wahitimu watarajiwa wa Kidato cha Nne wa skuli hiyo katika risala yao walieleza kwamba elimu waliyoipata ya Kidato cha Nnne imewapa misingi imara ya kujiunga na Elimu ya Juu pia, kuwajengea uwezo wa kujitambua na kufikiria kabla ya maamuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba (wa tatu kutoka kulia) akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kada maalum ya michezo katika Skuli ya Sekondari ya Jambiani wakati wa hafla ya mahafali hayo. Skuli hiyo ndiyo pekee katika mkoa inayofundisha kada hiyo.

Katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Wilaya aligawa vyeti maalum kwa wanafunzi wa Michezo pamoja na kushuhudia sanaa mbali mbali zilizotumbuizwa na wanafunzi wa skuli hiyo ikiwemo utenzi, nashid, mashindano ya kukuna nazi pamoja na kipaji kilichooneshwa na mwanafunzi mwenye mahitaji maalum wa skuli hiyo.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Mwakilishi, Mbunge pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news