Mzee Salim awashirikisha jambo wanahabari nchini

NA DIRAMAKINI

MJUMBE wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amewataka wanahabari nchini kusoma sheria zinazohusu masuala ya habari na nyingine.
Lengo likiwa ni kupata uelewa mpana ambao utawawezesha kufahamu na kushauri mahali ambapo wanataka zifanyiwe marekebisho kwa ustawi bora wa tasnia hiyo hapa nchini.

Mzee Salim anatoa wito huo ikiwa tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.
“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Akizungumza Oktoba 21,2022 jijni Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wahariri juu ya mipango ya uchechemuzi wa mabdiliko ya sheria za habari, Mzee Salim amesema, mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari ataweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wabunge na kuwashawishi juu ya sheria zinaminya uhuru wa habari na haki za binadamu.

“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa,” amesema

Kwa upande wake mwezeshaji, Tumaini Mbibo amesema, ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.

Amesema, haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo hivyo vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko.
Kwa uapnde wake Sylvester Hanga amesema, waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa.

“Waandishi wa habari ni lazima wawe mstari wa mbele kuisemea jamii lakini ni lazima wahakikishe sheria zinazominya uhuru wa habari zinafanyiwa marekebisho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

Aidha, Joyce Shebe amesema anaamini wahariri wakijua namna ya kushawishi watunga sheria, sera na mipango ya Taifa watakuwa kwenye nafasi njema ya kuchochea maendeleo ya mtu mmoja na Taifa.
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema, wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,”amesema Balile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news