TANZANIA HII SIMBA, TUKUBALI TUKATAE

NA LWAGA MWAMBANDE

NI zaidi ya miaka 80 ya ukongwe wa Klabu ya Simba, klabu ambayo tangu kuanzishwa kwake, licha ya kupitia changamoto mbalimbali imeendelea kuimarika mwaka baada ya mwaka.

Kuimarika huko kumeifanya klabu hiyo kuendelea kuyamudu vema mazingira ya soka la ndani na nje ya nchi. Pengine kwa sasa, unaweza kutamka au kukiri wazi kuwa, Simba SC ni shujaa wa soka la Tanzania na Kimataifa kwa upande wa wanaume na wanawake.

Ushujaa huo unatokana na sababu mbalimbali, kwa uchache, klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimabazi jijini Dar es Salaam,imekuwa ikiiwakilisha vema Tanzania katika anga za Kimataifa.

Mosi, ni kupitia wachezaji wa Simba katika soka la wanawake na wanaume wameendelea kuwa vinara duniani,kumbuka mchezaji wa kwanza toka Tanzania kufunga bao Kombe la Dunia la Wanawake chini ya Umri wa Miaka 17 (World Cup U17) kupitia Timu ya Taifa ni Diana Mnally kutoka Simba Queens.

Pili, mchezaji wa kwanza toka Tanzania kuchaguliwa kuwa nyota wa mchezo wa Kombe la Dunia la Wanawake chini ya Umri wa Miaka 17 (World Cup U17) kupitia Timu ya Taifa ni Violeth Nicholas kutoka Simba Queens.

Tatu, wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambao wameendelea kufanya vema ni Simba SC huku Soka la Wanawake Kimataifa wakiwa vinara Simba Queens bila kusahau bao bora la Afrika ambalo lilifanikishwa na Pape Ousmane Sakho wa Simba SC, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema;

1. Simba, Simba Simba Simba,
Inayotamba ni Simba,
Ndani na nje ni Simba,
Tukubali tukatae.

2. Zinazosomeka namba,
Orodha hiyo ya Simba,
Tunang’aa tunatamba,
Tukubali tukatae.

3. Kombe la Dunia Simba,
Nako huko inatamba,
Ona rekodi za Simba,
Tukubali tukatae.

4. Ni Mchezaji wa Simba,
Diana kutoka Simba,
Tanzania imetamba,
Tukubali tukatae.

5. Goli la kwanza la Simba,
Kombe la Dunia Simba,
Akafunga mwanasimba,
Tukubali tukatae.

6. Mchezaji alotamba,
Kwenye mechi kuwa mwamba,
Kombe la dunia Simba,
Tukubali tukatae.

7. Violeth toka SImba,
Uwanjani alitamba,
Kutagwa bora wa Simba,
Tukubali tukatae.

8. Kombe la Mabingwa Simba,
Afrika tuna Simba,
Timu ngeni yazilamba,
Tukubali tukatae.

9. Kimataifa ni Simba,
Miaka kadha ni mwamba,
Kote waiimba Simba,
Tukubali tukatae.

10. CAF wanawake Simba,
Huko twaenda waimba,
Watuwakilisha Simba,
Tukubali tukatae.

11. Serengeti Girls Simba,
Na wengine wanatamba,
Kwenye mechi wawaimba,
Tukubali tukatae.

12. Afrika timu Simba,
Kotekote zinatamba,
Kimataifa twaimba,
Tukubali tukatae.

13. Ni uwekezaji Simba,
Unafanya tukatamba,
Mo kaipaisha Simba,
Tukubali tukatae.

14. Hao viongozi Simba,
Wanafanya ya kubamba,
Hiyo yainuka Simba,
Tukubali tukatae.

15. Na ilikotoka Simba,
Nenda ukapange chumba,
Mzazi ikae mimba,
Tukubali tukatae.

16. Liteseka sana Simba,
Na hata kuchekwa Simba,
Sasa siyo ile Simba,
Tukubali tukatae.

17. Timu kusikia Simba,
Kwao huwa jambajamba,
Jinsi inatamba Simba,
Tukubali tukatae.

18. Bara Afrika Simba,
Inazidi panda Simba,
Kwa ubora inatamba,
Tukubali tukatae.

19. Ya kumi na moja Simba,
Ubora wanaiimba,
Uwanjani inatamba,
Tukubali tukatae.

20. Wachezaji wetu Simba,
Jinsi wanagawa vyumba,
Kotekote twawaimba,
Tukubali tukatae,

21. Tanzania hii Simba,
Inaifanya kutamba,
Kotekote waiimba,
Tukubali tukatae.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news