Dkt.Ishengoma:Maandalizi mashindano ya Urembo ya Utanashati ya Viziwi duniani yanaendelea vizuri

NA ADELADIUS MAKWEGA

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya Utanashati na Urembo ya viziwi Duniani yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022 yanaendelea vizuri huku Watanzania wanaoshiriki katika mashindano haya wameendelea kufanya mazoezi kwa juhudi na bidii zote mwezi mzima sasa huko Bagamoyo hadi kilele cha mashindano hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa nchini, Dkt.Emmanuel Ishengoma katika kikao maalumu cha maandalizi haya kilichofanyika Oktoba 13, 2022 Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“Serikali tuna jukumu la kuhakikisha kwanza washiriki wa Tanzania wanajianda vizuri, wanashiriki na kushinda mashindano haya, tangu mwezi wa nane 2022 vijana wetu chini ya walimu makini wanawafundisha vijana hao watakaoshiriki shindano hilo wakijinoa katika lugha za alama, mitindo, mavazi na miondoko, wataendelea kuwa kambini hadi haya mashindano yatakapokamilika, wanafanya mazoezi kila siku asubuhi, mchana na jioni. Wakufunzi wetu wa sasa wena uzoefu mkubwa sana na wanawapa uzoefu huo wa kuweza kushinda mashindano haya ya kimataifa.”

Akitaja majukumu mengine ya Tanzania katika mashindano haya Mkurugenzi Dkt.Ishengoma amesema kuwa, maandalizi ya kupokea ugeni huo mkubwa yanaendelea vizuri sana kwa kushirikisha wadau mbalimbali na sasa Tanzania tunatarajia kuonesha fursa kadhaa tulizonazo za sanaa, utamaduni na utalii.

Akichangia katika kikao hicho cha maandalizi Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Zanzibar Dkt. Omar Abdalla Adam alisema kuwa ushiriki wa Zanzibar upo vizuri wamejipanga vema kupitia makundi maalumu na watakuwepo kushuhudia tukio hilo la kimataifa.

Wadau wakuu wa maandalizi ya mashindano haya waliwakilishwa na Habibu Mrope ambaye ni Rais wa Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Afrika na pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa kwa viziwi Tanzania (KISUVITA) na kikaoni hapo alisema kuwa anazishukuru sana serikali zote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwa nao jirani katika maandalizi ya mashindano hayo yatakayoanza Oktoba 28 na kukamilika Oktoba 30,2022 jijini Dar es Salaam na akijinasibu kuwa taifa letu litang’ara katika mashindano haya. “Watanzania ndugu zenu viziwi tunawawakilisha vema na huku ni ushindi tu.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news