Dkt.Kijazi:Kwa mshikamano wetu tutafanikisha makusanyo makubwa

NA GODFREY NNKO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amesema kuwa, wananchi wengi wapo tayari kulipa kodi na tozo mbalimbali za ardhi ila wanakumbana na changamoto ya umbali au mifumo ya kulipia.
Ameyasema hayo Oktoba 3, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao kazi kilichowakutanisha wadau kutoka benki mbalimbali na kampuni za simu ambao watashiriki katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Ardhi nchini.

Dkt.Kijazi amesema, wizara imeamua kupanua wigo mpana wa kuzijumuisha benki na kampuni za simu ili kwa ukubwa wao wa kutoa huduma waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi vijijini na mijini.

"Ila kwa mwaka wa fedha uliopita makusanyo hayakuzidi asilimia 60 na hii imetokana na ukweli kwamba bado kuna changamoto, unakuta utayari wa mwanachi kulipa kodi au tozo za ardhi upo, lakini umwambie asafiri kilomita 20 au 30 aende kulipa kodi anaona ni usumbufu, anakwambia (mwananchi) ni wajibu wako kunifuata nilipo kuliko mimi niache kazi zangu wakati mwingine nakuta utaratibu wa kulipa kodi hauko vizuri.

"Kwa malengo tuliyojiwekea ni kwamba kwa mwaka tunatakiwa tukusanye sio chini ya shilingi bilioni 200 na hicho ninaamini bado ni kiwango kidogo kwa sababu makisio yanatokana na uhalisia wa mifumo ya makusanyo, uelewa wa wananchi na taratibu nzima zilizowekwa za kukusanya mapato.

"Niseme tena, kwa changamoto zilizopo kwa mwaka tunakisia kwamba tunaweza kukusanya shilingi bilioni 200, lakini tukilenga mifumo mizuri na tukashirikiana vizuri kwa pamoja ninaamini hiyo shilingi bilioni 200 inaweza ikawa mara mbili au zaidi ya mara mbili tunaendelea kufanya tathmini kwa kuangalia mitandao yetu ya makusanyo,"amesema Dkt.Kijazi.

Dkt.Kijazi amewaeleza wadau hao kuwa,njia nzuri ya kuleta ufanisi katika kukusanya kodi ni kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu jinsi ambayo makisio ya kodi mbalimbali yataweza kufikiwa na kukubaliana jinsi ya kutekeleza ikiwa ni pamoja na mawakala wa benki na kampuni za simu kuwa na uelewa ili waweze kuelimisha wananchi.

"Pamoja na kwamba sekta mbalimbali zinakusanya mapato, lakini mapato haya yanapokusanywa yanapelekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali, kila sekta inakusanya inapeleka kwenye mfuko wa serikali kikubwa hapa ni kuelewa si kila huduma ya serikali inayotolewa inazalisha. Zipo sekta za uzalishaji, zipo sekta za huduma,"amesema Dkt.Kijazi.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu Dkt.Kijazi amesema, nia kubwa ya kupeleka ni kwamba zisaidie kutoa huduma kwa wananchi bila kujalisha zimetoka sekta gani na kwamba, "jinsi unavyokusanya ndio mchango wako unatambulika katika bajeti ya serikali na pia ni rahisi kuomba baadhi ya fedha hizo zirudi zisaidie kuendesha sekta ya ardhi.

"Kwa mwaka jana ukilinganisaha kiasi kilichokusanywa na kiasi ambacho tumepokea kama wizara unaweza kusema ni asilimia kati 60 au 70 zimerudi katika uendelezaji wa sekta ya ardhi kama nilivyosema tulikusanya kwenye shilingi bilioni 100 na zaidi, lakini tulipokea karibu shilingi bilioni 100 kama bajeti ya shughuli za uendelezaji wa sekta ya ardhi.

"Na bajeti hiyo imeelekezwa kwanza katika kuboresha maandalizi ya mipango miji katika maeneo yetu mbalimbali nchini na katika kufanya hivyo zipo huduma ambazo zinaendana na majukumu ya uendelezaji wa mpango miji, hii ni pamoja na kupima maeneo mbalimbali katika vijiji vyetu na pia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sekta ya ardhi katika maeneo yetu.

"Na katika kupima miji na kupanga maeneo mbalimbali kuna maeneo pia wananchi wanahitaji kufidiwa ili baadhi ya maeneo yaweze kuachwa ambayo yanashughuli muhimu za kitaifa. Ili serikali iweze kufanikiwa inabidi baadhi ya wananchi wapewe fidia wapishe maeneo yao mojawapo ya maeneo ambayo tumepata bajeti ni kufanya tathmini na kuweka mfumo mzuri,"amesema Dkt.Kijazi.

Akizungumzia, kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kiwango kinachotakiwa hususani halmashauri zote nchini, Katibu Mkuu huyo amesema kwamba serikali itawapa motisha kwa mujibu wa taratibu za kiserikali na haitawaacha mbali wadau wote muhimu kufanikisha jambo hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo na taifa kwa ujumla.

"Kikao hiki ni mwendelezo ambao tumeufanya na viongozi mbalimbali, tumefanya kikao na wakurugenzi wa majiji, miji na halmashuri zetu. Mojawapo ya masuala tuliyoambiana ni umuhimu wa halmashauri kuongeza nguvu na kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ya sekta ya ardhi walikuwepo viongozi wa TAMISEMI na viongozi wa Wizara ya Ardhi, hivyo zile halmashauri ambazo zinafanya vizuri upo utaratibu wa kiserikali,"amesema Dkt.Kijazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news