EBOLA,TUCHUKUE TAHADHARI:Kama wewe msafiri, ulipita kwa jirani

NA LWAGA MWAMBANDE

UGONJWA wa Ebola ni miongoni mwa magonjwa hatari duniani, ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vujulikanavyo kitaalam kama 'Ebola Virus'.

Aidha, ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama homa za virusi zinazosababisha kutoka damu sehemu za wazi za mwili mfano puani, masikioni na machoni. Ugonjwa huu unaathiri binadamu na wanyawa kama vile nyani, ngedere, sokwe na popo.

Tafiti zinaonesha kuwa, kwa nyakati tofauti mlipuko mkubwa kuwahi kuokea duniani umetokea katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Mlipuko huo pia umeaziathiri nchi za Nigeria, Senegal, Mali,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Marekani, Uhispania na hivi karibuni nchini Uganda.

Lwaga Mwambande ambaye ni mshairi wa kisasa anasema, kutokana na muingiliano kati ya nchi na nchi, kuna uwezekano mkubwa wa ugonjwa huu ukaenenea nchi nyingine endapo tahadhari hazitachukuliwa, endelea;


1:Tukubali tukubali, hatari iko njiani,
Tufanye ya kukabili, isifike malangoni,
Ni karibu siyo mbali, walioko msambweni,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii ebola.

2:Uganda wanateseka, tayari wa hatarini,
Sasa wanahangaika, mijini na vijijini,
Ugonjwa kudhibitika, wabakie na Amani,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii ebola.

3:Kama wewe msafiri, ulipita kwa jirani,
Kule kuliko hatari, nawe wahisi mwilini,
Haraka funga safari, fika hospitalini,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

4:Kama unazo dalili, wajisikia mwilini,
Kwamba una homa kali, yakusumbua mwilini,
Kichwa chauma vikali, kimbia sipitalini,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

5:Unaumwa huna hamu, hivyo viungo mwilini,
Tena unatokwa damu, sehemu wazi mwilini,
Usijebakia homu, nenda hospitalini,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

6:Huu ugonjwa hatari, hapa kwetu duniani,
Bila yetu tahadhari, tutajiweka shidani,
Tusije tukasubiri, tunapokosa Amani,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

7:Pamoja na haya yote, ambayo yako hewani,
Tuyasikilize yote, maonyo kwetu nyumbani,
Tusijebweteka wote, ugonjwa uje nyumbani,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

8:Vituo vya mipakani, tukiwapo safarini,
Ni vema kuwa makini, tukiwa nao wageni,
Kujichanganya mwilini, twajitia hatarini,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

9:Wataalamu kotekote, tayari wako kazini,
Wanafanya mambo yote, tusijikute shidani,
Tufuatilie yote, kwa usalama nyumbani,
Tuchukue tahadhari, dhidi ya hii Ebola.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments