HAYAWI HAYAWI HUWA:Mwendokasi sasa kweli, treni tutajinoma

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 25, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa mabehewa mapya kwa ajili Reli ya Kisasa (SGR) ya Shirika la Reli Tanzania yanayotengenezwa na Kampuni ya Sung Shin Rolling Stock (SSRT) iliyoko nchini Korea Kusini.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, kati ya mabehewa 81 ambayo Tanzania inatengeneza kutoka kampuni hiyo, tayari 36 yamekamilika na yameshaletwa nchini na 45 yaliyobaki yanategemewa kukamilika Machi, 2023.

Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea kampuni ya SSRST inayotengeneza mabehewa na injini za treni nchini Korea Kusini huku akisisitiza hayo ni mabehewa ya daraja la tatu na yatatoa huduma zote muhimu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,SRG ambayo ni ufupisho wa neno la Kiingereza Standard Gauge Railway ambayo inatekelezwa kwa ufanisi hapa nchini, ikikamilika mambo yatakuwa mazuri zaidi kupitia sekta ya usafirishaji, endelea;


1:Mwendokasi sasa kweli, treni tutajinoma,
Reli ya kisasa kweli, itaanza kuzizima,
Mabehewa ni kamili, PieM amesema,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

2:Yako themanina moja, Waziri Mkuu sema,
Thelathina sita yaja, nanga ni Darisalama,
Na hayo tunayo haja, Dar-Moro-tu-Dodoma,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

3:Tunangojea kwa hamu, bora kama tukisema,
Kusafiri tutadumu, muda ndio unasema,
Kwenda kurudi kwa zamu, bila simamasimama,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

4:Mambo ya Serikali yetu, tunaona tunasoma,
Kwa hii miradi yetu, haijawahi simama,
Ni ahadi zake kwetu, yatenda iliyosema,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

5:Rais lisisitiza, Samia Suluhu mama,
Miradi kuendeleza, hadi kufika hatima,
Dalili zajieleza, yatendeka alosema,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

6:Treni ya mwendokasi, mradi dunia nzima,
Kula pesa kama hasi, jinsi zinavyoyoyoma,
Ujenzi wenda kwa kasi, taarifa twazisoma,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

7:Sasa tunasubiria, gari-umeme twasema,
Tutakalolitimia, kusafiri kwa salama,
Kasi tunafurahia, saa chache wanasema,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

8:Yanapotendeka haya, tuonayo na kusoma,
Nasi tusione haya, kwa watu tukisimama,
Kwamba dola iko faya, inatenda inasema,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

9:Waziri mkuu wetu, kasikika akisema,
Mabehewa hayo yetu, yaja tusishike tama,
Hiyo reli nzuri yetu, wengi namba watasoma,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

10:Kongole kwa Serikali, mnatenda mlosema,
Kwa treni ni wa kweli, kifua mbele simama,
Taratibu toka mbali, twarejea twasimama,
Treni ya mwendokasi, hayawi hayawi huwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments